NA MWAJUMA JUMA

TIMU ya soka ya Elhila juzi ilifuta makosa yake na kufanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Muembemakumbi katika mfululizo wa ligi daraja la pili wilaya ya mjini, inayoendelea katika viwanja vya Mao Zedong.

Elhila ambayo ilitanguliwa kufungwa ilijitahidi kupapatua na kufanikiwa kuondoka na ushindi huo, baada ya wachezaji wake Ramadhan Miraji na Khamis Hassan kufunga mabao hayo huku bao la kufutia machozi la Muembemakumbi likifungwa na Sadiq Abdilahi.

Katika mchezo uliopita Elhila ilifungwa na timu ya Dangers mabao 5-1 mchezo ambao ulichezwa kwenye uwanja wa Mao Zedong.

Mchezo mwengine uliochezwa hapo juzi ulikuwa ni kati ya Dangers Pulling Land ambao ulimalizika kwa Danger kushinda mabao 2-1 ambayo yote yalifungwa na Joel Yuda dakika ya 73 na 85 na Pulling land lilifungwa na Mohammed Juma Philipo dakika ya 20.

Ligi hiyo leo inatarajiwa kuendelea tena kwa kuchezwa michezo minne ambapo katika uwanja wa Mao Zedon A GS itacheza na West Coast saa 8:00 mchana, saa 10:00 Sebleni itapambana na Meya City, wakati katika uwanja wa Mao Zedong B saa 8:00 mchana Ajax itacheza na Maruhubi na Magomeni itaikaribisha University saa 10:00 za jioni.