‘ELIMU ni ufunguo wa maisha’ msemo huo ni maarufu sana katika mwambao huu wa Afrika Mashariki na kwamba umekuwa ukitumika sana kutokana na umuhimu wa elimu katika maisha ya wanaadamu hapa duniani.
Suala la umuhimu wa elimu ni pana sana kwani vitabu vya dini vimeeleza wazi jinsi ya wanaadamu kujifunza elimu ya dini na ya dunia.
Ni ukweli usiopingika kuwa mwenye elimu si sawa na asiekuwa na elimu kwa njia yoyote ile na ndio maana tukaamrishwa kujifunza.
Kwa mukhtaza huo basi makala yetu hii itazungumzia umuhimu wa elimu kwa misingi inayohitajika.
Hivyo, jamii yoyote inahitaji misingi na nguzo za kuisimamisha na kuipa uhai na ustawi. Misingi hiyo na nguzo hizo hatuwezi kuzipuuza tukitaka kujenga jamii yenye mafanikio na maendeleo. Bila shaka jamii ni kama mwanadamu inaathirika kwa mambo yanayojiri na hali inavyotukia, mambo na hali ama ni za mguso au za kufikirika tu, la muhimu ni kwamba ukweli huu unatupa uelewa wa kuwa tuna uwezo wa kubadilisha hali tunayo kwa hali iliyo bora na kuondoa mabaya na kuepukana na maovu.
Pia, la kuzingatiwa kwamba hatuwezi kuboresha jamii na kuendeleza hali ni kwamba kuna mambo yanayochangia kufanikiwa kwa juhudi hizo za uboreshaji mambo haya ni nguzo muhimu zinazojenga jamii na kumsaidia mwanadamu apate maisha mazuri yenye amani na utulivu.

Nguzo za kujenga jamii ziko nyingi kwa viwango mbalimabli kuanzia mtu binafsi kisha familia, kaya, ukoo, kabila na jamii nzima. Kila nguzo miongoni mwa nguzo hizo ina majukumu, nafasi na umuhimu wake kujenga jamii. Kwa mtu binafsi, anatakiwa kubeba jukumu lake katika jamii ama kwa kujifunza au kufundisha, kuchangia kwa kiasi kinachowezekana kukuza jamii na kuendeleza maisha yake yeye na maisha ya wenzi wake. Kila mtu huwa na wajibu wa kujifunza elimu yenye manufaa kidini na kidunia, kisha kutekeleza mafunzo aliyoyapata katika maisha yake kwa mujibu wa hali halisi ya mambo kwa ajili ya kunufaika na kunufaisha kwa mafunzo yale.
Pia, mtu anatakiwa kujifunza elimu na mafunzo yasiyo ya skulini na vyuoni tu, bali afadhali kujifunza namna ya kuamiliana na watu, kuwa mtu mwenye heri kwa nafsi yake, jamaa zake, jamii yake na nchi yake. Awe mtu mwenye mchango, athari na mikono ya kuwasaidia wengine kwa misaada ya kila aina si lazima iwe misaada ya fedha tu, ambapo kuna misaada muhimu zaidi kuliko fedha.
Vile vile, mtu anatakiwa kuheshimu maadili anayopewa na kulelewa tangu utotoni mwake mpaka mazikoni, kwani maadili haya wakati wengi huwa sheria na katiba ambayo lazima ifuatwe na wanajamii wanaoishi pamoja.
Maadili haya yanachangia kwa kiasi kikubwa kuidhibiti jamii na kuweka mipaka inayoilinda jamii husika isisambaratike wala kuporomoka. Haya maadili yanakuwa yakitokana na dini, mila na desturi, urithi, utamaduni na hata mwingiliano baina ya jamii moja na nyingine. Kwa kuwa maadili haya yanachukua nafasi ya kanuni na sheria, yanastahili kuheshimiwa na kutunzwa vizuri kwa lengo la kuunda jeshi la ulinzi wa tabia na dseturi za jamii. Kwa hali hii tunabainika kwamba maadili yanachangia sana kumwelekeza mtu kwenye njia iliyo sahihi.
Kwa hakika, mtu ye yote hawizi kuishi maisha ambayo yanakwenda sambamba na maumbile na malengo ya Mungu kuumba na kuanzisha ulimwengu huu, pasipo na kuwa na vyanzo viwili vya msingi; elimu na maadili. Kwani vyanzo hivyo viwili vina athari kubwa mno kuunda wanajamii na kuweka jamii katika kiwango chake ama cha juu au cha chini. Hali hiyo hiyo ya mtu huwa ya jamii nzima ambapo mtu ni sehemu ndogo zaidi kuliko ya jamii ambaye huwa jiwe la msingi la kujenga jamii yote.
Kwa urefu zaidi, hebu tuangalie hali ya nguzo hizo muhimu yaani; elimu na maadili na mchango wao katika kuimarisha jamii nzuri na kuangalia namna ya kuziendeleza jamii zetu za kiafrika kwa kutegemea nguzo hizo mbili kwa lengo la kujenga jamii bora.
Pasipo na kuzingatia elimu, jamii inaweza kuyumba katika dhulma ya ujinga, maradhi na maovu ya kila aina, kwani asiyejua husababisha madhara na majanga kwake mwenyewe na kwa umma wote, kwa hiyo elimu ikawa msingi wa kwanza wa kujenga jamii bora.
Pia, jamii inayozingatia elimu hufikia viwango vya juu vya mafanikio na maendeleo kwa kuwa elimu ndiyo silaha ya kuitetea jamii na kuiokoa kutokana na mabaya mengi na mengi. Bila ya kuibagua jamii kwa misingi ya dini, rangi, siasa, madhehebu au sifa yoyote nyingine, jamii zetu za kiafrika zinatakiwa kuangalia namna ya kufaidika kwa elimu kujiendeleza na kuboresha hali yake na wananchi wake kama zilivyofanya jamii nyingine nyingi katika nchi mbalimbali duniani.

Kimsingi, elimu bora ndiyo mwanga wa kuongoza mtu na jamii kwenye masilahi yake na kuonyesha hatari na maovu na namna ya kuepukana nayo, kwa hiyo hakuna mwenye akili hata mmoja anayeweza kupuuza umuhimu wa elimu bora kuwaokoa wanadamu kutoka shari na mabaya na kama tukiangalia jamii zilizopata maendeleo na kuhakikisha ustawi wa kweli tutatambua kuwa msingi wa mafanikio yao ni kutegemea mfumo mzuri wa elimu kuanzia awamu ya shule za msingi mpaka vyuo vikuu, ule mfumo una sifa maalumu kama vile; usawa baina ya watu wote katika haki ya kupata hadhi yao ya elimu na kutenga hela za kutosha kwa ajili ya kuendeleza hali ya elimu nchini. Pia, kuandaa mazingaira mwafaka ya kutoa elimu yenye hali ya juu, jambo linalohitaji ushrirkiano mkubwa baina ya pande husika zote kwani serikali haihusiani peke yake kuendeleza hali ya elimu bali wananchi pia ambapo wanatakiwa kuzingatia wajibu na majukumu yao kutekeleza miradi ya serikali kuboresha hali ya elimu.
Inafahamika kuwa asasi yoyote ya kutoa elimu inategemea vipengele kadhaa katika shughuli za kufanikisha mikakati yake, miongoni mwa vipengele hivyo, walimu, mitalaa, vifaa vya kufundisha, wanafunzi na wazazi. Washiriki wa zoezi hilo la kutoa elimu na mafunzo wangejitahidi na kila mmoja angetimiza majukumu yake ipasavyo, zoezi zima la mafundisho lingefaulu. Ama ingetokea uzembe na dosari lolote, basi mambo hayatakuwa mazuri hivyo jamii nzima kukosa mwangaza na dira ya kuielekeza kwenye njia sahihi.
Na kwa kuthibitisha umuhimu wa elimu katika juhudi za kujenga jamii tunaweza kugundua mbinu za kuleta maendeleo ya jamii kupitia elimu, bali tunaweza kuchagua mfumo wa elimu uanofaa hali ya jamii na watu wanaoishi humo. Aidha, kupitia elimu tunaweza kutetea uhuru wa jamii.
Zaidi ya hayo, elimu inachangia kuziepusha jamii maovu na mabaya yanayoibuka kwa kuwapa wanajamii uelewa wa kutosha kuwakinga na ushawishi wowote na kuwasaidia waepukane na fikra mbaya bali inawaunga mkono kupinga fikra zisizo sahihi na kupambana nazo kwa kutegemea silaha ya elimu.
Kwa kweli, majanga mengi yanayotukia katika ulimwengu wetu wa kisasa yanatokana na ujinga na kutojali elimu na uboreshaji wake, ambapo maradhi mbalimabli yalijitokeza kwa sababu ya vitendo vibaya visivyo na msingi woowote wa kitaaluma. Isitoshe, bali mabaya mengine mengi yanayozisumbua jamii za kisasa yametokana na ukosefu wa elimu, jambo ambalo jamii nyingi zimeanza kulitambua mwishoni zikaanza kuzingatia elimu kwa kukiri kuwa njia ya pekee ya kupambana na mabaya haya ni elimu.
Kwa jumla, nchi au jamii yoyote inayotafuta maendeleo na mafanikio haina budi kuipa shime elimu na kuwaheshimu wataalamu wake na kufanya juhudi za kutosha za kuendeleza hali yake katika elimu. Hali halisi tunayoishuhudia katika enzi yetu ya kisasa inathibitisha kuwa uhusiano uliopo baina ya elimu na maendeleo na ustawi ni uhusiano mkubwa na wa uhakika kwani elimu ni kama ngazi ya kupanda wa kiwango cha juu na kuendeleza hali ya mtu na jamii.
Tunahitimisha kwa kupendekeza wanaadamu kuzingatia elimu inayotegemea mbinu za kisasa na kutojibana katika mifumo ya kijadi tu, bali tuhimize kugundua mbinu, vifaa vya kitaaluma na kufaidika kwa walioyafikia wengine ndani ya nchi yetu au nje kwa mujibu wa manufaa ya jamii na maslahi za watu wake.
Aidha, tungependa kusisitizia ukweli wa kwamba elimu haiwezekani
kubanwa na kuhusishwa katika aina maalumu ya elimu (Taaluma za Dini au Sayansi
za Kidunia) bali, elimu tunayoikusudia kwa makala yetu hii ni elimu ya
kunufaisha binadamu wote, ni elimu inayojenga vizazi wa kesho watakaokuwa na
jukumu la kujenga jamii zao binafsi na kuandaa mustakbali nzuri kwa kizazi
kijacho ili kujiokoa na kujilinda kutokana na maovu na madhara ya aina yoyote
hapa duniani na akhera twendako.
Imeandaliwa na;
Alaa Salah Abdulwahed
Mwalimu Msaidizi wa Kiswahili Chuo Kikuu cha Al-Azhar