TOKYO, Japan

MCHEZAJI wa timu ya taifa ya Kenya Harambee stars Michael Olunga amesema ataendelea kuangalia mbali zaidi baada ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), kutambua kipaji chake na kumuweka katika orodha ya wanasoka watano bora ambao hawajajulikana sana licha ya kuwika katika mwaka 2020.

 Olunga amesema licha ya kupokea ofa nyingi za kujiunga na timu mbalimbali barani Ulaya, lengo lake kwa sasa kubaki nchini Japan.

 Hata hivyo, wakala wake yuko huru kutathmini hali ilivyo kabla ya kushauriana naye kuhusu maamuzi mengine muhimu kimchezo.

Olunga aliwahi kufichua  kiu ya kuingia katika usajili rasmi wa timu ya Arsenal ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) chini ya kocha wa zamani wa kikosi hicho, Arsene Wenger.

Lakini hakuwa na bahati hiyo. Nyota huyo wa zamani wa Gor Mahia alijivunia msimu wa kuridhisha katika Ligi Kuu ya Japan (J1 League) na akatawazwa Mchezaji Bora na Mfungaji Bora wa msimu huu baada ya kucheka na nyavu mara 28 kutokana na mechi 32.