NA MADINA ISSA

MWENYEKITi wa Kamati ya siasa ya Mkoa wa Kusini Unguja, Rashid Hadid Rashid, amewataka wanachama wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) mkoani humo kutoa mashirikiano kwa serikali kupiga vita Ufisadi, Rushwa, wizi, ubadhirifu wa mali za umma pamoja na vitendo vya udhalilishaji.

Alisema serikali ya awamu ya nane inayoongozwa na Dk. Hussein Ali Mwinyi, imedhamiria kuondoa mambo hayo, hivyo wanachama wa jumuiya hiyo na wananchi watakuwa na mwamko wa kutoa taarifa za viashiria vya kuwepo kwa matendo hayo, kutarahisisha upatikanaji wa watu wanaotenda matendo hayo na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Aliyasema hayo alipokuwa akifungua mkutano wa baraza la Jumuiya hiyo uliofanyika katika Ukumbi wa Kibeshi, Unguja Ukuu Mkoani humo na kueleza kuwa ni vyema wanachama hao kujiandaa kikamilifu na uchaguzi wa ndani ya chama ifikapo 2022.

Alisema maandalizi hayo yatapelekea kupatikana viongozi wenye uwezo wa kukiweka madarakani chama hicho kwenye uchaguzi mkuu wa 2025 sambamba lakini pia kumuunga mkono Dk. Mwinyi kutekeleza maridhiano ya kisiasa ambayo ndio chanzo cha ushindi wa CCM katika chaguzi zijazo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa UWT mkoani humo, Shemsa Abdalla Ali, aliwataka wanawake kujitokeza kujiunga na jumuia hiyo sambamba na kulipa ada kwa wakati jambo litakaloipa jumuiya uhai na uwezo wa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Akitoa taarifa ya jumuiya hiyo, Katibu wa jumuiya hiyo, Asha Mzee, alisema mafanikio yaliyopatikana ndani ya mkoa huo kupitia kazi za jumuiya hiyo ikiwa ni pamoja na kuwaunganisha wanawake wa mkoa huo kuwa wamoja.

Asha alieleza mafanikio mengine kuwa ni kuwajengea uwezo wa kuthubutu kukipigania chama katika uchaguzi uliopita na kugombea nafasi mbalimbali za uongozi wa chama na serikali.

Kwa mujibu wa kalenda ya utekelezaji wa shughuli zake, kikao cha baraza kuu la UWT katika mkoa huo hufanyika kila baada ya miezi sita ambapo hutanguliwa na vikao vya mabaraza ya UWT vya wilaya mbili za mkoa huo, wialaya ya Kati na Kusini Unguja.