NA TATU MAKAME

UMEFIKA wakati kwa asasi za kiraia nchini kuhamasisha jamii kuchangamkia fursa zilizomo katika sekta ya uvuvi ili kuwa na mafanikio ya kiuchumi, kuwaongezea kipato na   kuondokana na tatizo la ajira.

Wito huo umetolewa na Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi, Mgeni Hassan Juma, alipokuwa akifunga tamasha la 14 la asasi za kiraia Zanzibar lililofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abulwakil Kikwajuni, Zanzibar.

Mgeni alieleza kuwa Zanzibar ikiwa inatekeleza sera ya uchumi wa buluu, wananchi wengi wanaweza kutumia sekta zilizomo katika sera hiyo ili kujikomboa hivyo ipo haja kwa AZAKI kuishajihisha jamii kuingia katika uchumi huo.

Alisema hilo linawezekana kwa kuwa asasi za kiraia zimejenga imani kwamba serikali ya Mapinduzi Zanzibar ina nia ya dhati kabisa ya kuweka mazingira mazuri kwa asasi hizo kutekeleza dhamira ya kiuchumi.

Aidha alisema asasi hizo zina jukumu la kuwaunganisha wananchi na serikali yao katika kujiletea maendeleo na kuchochea kasi ya mabadiliko ya kiuchumi.

Wakati huohuo Naibu Spika Mgeni alizitaka asasi kuendelea kuwaunganisha wananchi katika kuzifikia fursa za maendeleo ya kiuchumi na kijamii kupitia shughuli zao bila kukiuka sheria za nchi.          

Alifahamisha kuwa asasi za kiraia zinaitegemea serikali na serikali inazitegemea katika kupanga mipango ya maendeleo na kuiwezesha jamii kufahamu tafsiri sahihi ya mipango ya maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa jamii.

Alizitanabahisha asasi hizo kuendelea kutumia uzoefu wao katika midahalo hiyo ya muda mrefu katika kutekeleza dhima ambayo inalenga kufikia ustawi wa jamii wa Zanzibar.

Hata hivyo alilipongeza shirika la ‘The Foundation for civil society’ kwa kusaidia ufadhili wa tamasha hilo muhimu na kulitaka kuendelea kuzisaidia asasi za kiraia katika kutekeleza majukumu yake hasa kutokana na kazi zao wanazofanya za kuisaidia jamii kuwa kazi zao zinathaminiwa sana na serikali.

Mapema wakiwasilisha mada mbalimbali kwenye tamasha hilo Dk. Juma Malik Akili na Dk. Mzuri Issa na wataalamu kutoka mamlaka mbalimbali walisema uwepo wa asasi za kiraia umeleta mabadiliko ya kiuchumi kwa kuibadili jamii katika kupiga hatua za maendeleo.