Kuapishwa Jan 20

BAADA ya vurugu kutokea kwenye majengo ya bunge mjini Washington, hatimaye Baraza la Wawakilishi na Baraza la Seneti limeidhinisha ushindi wa Joe Biden kuwa Rais na Kamala Harris Makamu wa Rais wa Marekani.

Mchakato wa kuthibitisha ushindi huo katika kikao cha pamoja cha mabaraza hayo, ulivurugwa na kundi la wafuasi wa Rais anayeondoka madarakani, Donald Trump ambao waliyavamia majengo ya bunge hilo.

Hatua ya kuidhinishwa, kwa kawaida huwa ni utaratibu wa haraka na ni hatua ya mwisho ya kuthibitisha uchaguzi wa Urais kwa mujibu wa Katiba ya Marekani.

Akitangaza matokeo hayo, Seneta wa Minnesota kupitia chama cha Democratic Amy Klobuchar, , ambaye alikuwa miongoni mwa waliosimamia mchakato mzima wa kura, amesema democratic imeshinda, ambapo jumla ya matokeo rasmi ya kura za wajumbe ni 538, ambazo Biden amepata kura 306 na Trump 232.

”Rekodi tunayoiweka hapa ni kwamba Joe Biden atakuwa Rais na Kamala Harris Makamu wake kulingana na kura ambazo tumepewa.” alisema Klobuchar.

Kura za wajumbe zilithibitishwa baada ya mabunge yote mawili, yaani lile la uwakilishi na lile la seneti kukataa pingamizi kuhusu kura zilizopigwa katika vituo vya jimbo la Pennsylvania na Arizona.

Ushindi huo ni mkubwa sana kwa chama cha Demokratic kwani hivi sasa wanachama wa Democratic kwa mara ya kwanza, tangu awamu ya kwanza ya utawala wa Barack Obama watashikilia udhibiti wa mabaraza mawili ya bunge na Ikulu ya  White House.

Makamu wa Rais Mike Pence alikuwa wa kwanza kuzungumza katika kikao hicho cha pamoja cha mabaraza yote mawili kama Rais wa Baraza la Seneti baada ya kuahirishwa kwa muda kutokana na vuguvugu hilo lililotokea Bungeni hapo.

Makamu wa Rais Pence alisema, “Leo ilikuwa siku ya kiza katika historia ya bunge la Marekani, lakini ninatoa shukurani kwa juhudi za haraka za polisi wa bunge, wakishirikiana na polisi wa serikali kuu na wale wa hapa mjini kukomesha ghasia hizo.”

Baada ya kuanza tena kwa kikao hicho, kiongozi wa wengi kwenye Baraza la Seneti, Mitch McConnel alilaani ghasia hizo na kuthubutu kusema waliojaribu kuivuruga demokrasia wameshindwa.

Hata hivyo, mchakato wa kuidhinisha ushindi wa Biden ulikumbwa na ucheleweshaji wa muda mrefu, kutokana na vizingiti vilivyowekwa na wanachama wa Republican kutaka kuhesabiwa upya kura kwenye majimbo ambayo Biden alishinda, ingawa madai hayo yalitupiliwa mbali.

Baada ya ushindi wa Biden kuidhinishwa rasmi na Baraza la Wawakilishi na Baraza la Seneti, Rais Trump amesema kutakuwa na kipindi cha mpito kilichoratibiwa mnamo Januari 20.

Ushindi huo ni pigo kubwa kwa Trump katika juhudi zake za kumzuia Biden kutwaa mamlaka baada ya kuwasilisha kesi mahakamani na kuwalimbikizia wajumbe presha ya kubatilisha matokeo hayo.

Naye Rais Mteule Joe Biden akiwa nyumbani kwake Delaware alilihutubia taifa na kulaani ghasia na kusema ameshtushwa na kuskitishwa na tukio hilo.

Biden alisema, “Kuvamia jengo la bunge na kufanya uhalifu mbali mbali kama kuvunja madirisha kukalia ofisi za wabunge, kuingia ndani ya baraza la seneti na kuharibu madawati na vitu vya maafisa wa bunge, kutishia usalama wa watu waliochaguliwa, hayo si malamamiko ya amani bali huo ni uasi.”

Biden aliongeza kwa kusema, “Kama tukio hilo la waandamanaji ingekuwa ni maandamano yaliyofanywa na kundi la watu weusi ‘Black Lives Matter’ hatua zilizochukuliwa dhidi yao zingekuwa tofauti kabisa ikilinganishwa na walivyochukuliwa wahuni waliovamia bunge.”

Aidha katika kumbukumbu za hotuba yake mara baada ya ushindi na kuidhinishwa, mnamo Disemba 15, Biden alisema kwamba demokrasia ya Marekani ilikuwa imeingiliwa na kujaribiwa kwa majaribu mbali mbali lakini imedhihirisha kuwa ni jasiri, ya kweli na thabiti.

Biden pia aligusia misimamo wa Donald Trump ya kujaribu kupinga matokeo ya uchaguzi akisema kuwa katika historia ya Marekani, ni wananchi ndio huwapa wanasiasa mamlaka.

“Moto wa demokrasia uliwaka nyakati za zamani katika nchi hii, na tunafahamu kwamba hakuna lolote linaloweza kuuzima moto huo si majanga la ugonjwa wala ukiukaji wa mamlaka,” alisema Biden.

Wakati huohuo Rais Donald Trump ametoa taarifa akikubali kukabidhi madaraka kwa njia ya amani hapo ifikapo tarehe 20 mwezi huu, huku akirudia madai yake ya awali kwamba uchaguzi huo ulikumbwa na udanganyifu.

”Licha ya kwamba sikubaliani na matokeo ya uchaguzi na huo ndio ukweli, kutakuwa na shughuli ya mbadala ya kukabidhi mamlaka ifikiapo Januari 20 ”, alisema katika chapisho la msemaji wake lililochapishwa katika akaunti ya twitter.

”Nimekuwa nikisema mara kwa mara kwamba ni kura halali pekee zinahesabiwa, huku hatua hiyo ikiwakilisha mwisho wa kuifanya Marekani kuwa bora zaidi katika historia ya muhula wa Rais na ni mwanzo wa vita vya kuhakikisha tutaiboresha zaidi Marekani ”, aliongezea Trump.

Katika ujumbe uliochapishwa kwenye ukurasa wa Twitter wa Dan Scavino, ambaye ni mkurugenzi wa habari wa Trump, Rais huyo wa Marekani aliongeza kwa kusema ingawa hakubaliani kabisa na matokeo ya uchaguzi huo, hivyo kutakuwa na utaratibu ulioandaliwa wa kukabidhi madaraka.

Kwa mujibu wataarifa, Kampuni za mitandao ya kijami ya Twitter na Facebook kwa mara ya kwanza ziliifungia ukurasa wa Trump kwa siku moja kwa madai ya kukiuka sera zao mtandao.

Kwa hatua nyengine wapinzani wa Trump katika mabunge yote mawili wametoa wito kwa Rais huyo kuondolewa madarakani baada ya wafuasi wake kufanya uvamizi na vurugu hilo.

Seneta wa Democratic Chuck Schumer amesema, Trump anastahili kuondolewa mara moja, na ikiwa sio hivyo, Spika wa bunge la Wawakilishi Nancy Pelosi amesema anaweza kupigiwa kura ya kutokuwa na imani naye.

“Rais huyu hastahili kuendelea kushika hatamu hata kwa siku moja zaidi,” amesema Schumer, ambaye ataongoza chama cha Democratic chenye wabunge wengi katika Bunge la Seneti litakapoanza kikao kipya baadaye mwezi huu.

Amesihi kuwa, baraza la Trump kumuondoa madarakani kwa kutumia marekebisho ya katiba nambari 25 ya Marekani, ambayo yanaruhusu makamu wa Rais kuchukua uongozi ikiwa Rais ameshindwa kutekeleza majukumu yake kwasababu ya matatizo ya kiakili au kimwili.

Hatua hiyo itamhitaji makamu Rais Mike Pence na angalau wabunge wanane wa baraza la mawaziri kumpinga Trump na kutekeleza kifungu hicho cha katiba hatua ambayo hadi kufikia sasa imeonekana kutokuwa tayari kutekelezwa.

Kuondolewa kwa Rais huyo ni kupitia muswada uliotoloewa wa kutokuwa na imani naye, kutahitaji kuungwa mkono na wabunge wa Republican ambao kufikia sasa ni wachache tu wanaoonekana kutofautiana naye.

Mara baada ya Biden kuidhinishwa rasmi taarifa zinaeleza kuwa Rais huyo mteule wa Marekani, ametangaza rasmi kwamba atamteua Jaji Merrick Garland kuwa mwanasheria mkuu wa nchi hiyo.

Jaji Garland, ambaye kwa sasa ni jaji wa Mahakama ya Rufaa ya Washington, alipata umaarufu mwaka 2016 wakati ambapo Rais wa zamani wa Marekani Barack Obama alimteua kuwa Jaji wa Mahakama ya Juu kuziba nafasi iliyoachwa wazi kutokana na kifo cha jaji Antonin Scalia.

Hata hivyo, uteuzi huo ulipingwa na wabunge wa chama cha Republican ambao walikuwa wanadhibiti Baraza la Seneti.

Katika taarifa yake, Biden amesema Garland atasaidia kurejesha uhuru wa idara ya mahakama, ili ihudumie maslahi ya wananchi na sio ya Rais, sambamba na kurejesha tena imani ya umma katika utawala wa sheria na kufanya kazi bila kuchoka kuhakikisha mfumo wa Mahakama unakuwa wa haki na sawa.