NA MWAJUMA JUMA

KOCHA wa timu ya soka ya Jamhuri Mfaume Shaaban amesema wameondoka Pemba kuja Unguja, kushiriki michuano mapinduzi wala hawakuja kuuza wachezaji kwa kuonyesha ufundi.

Akizungumza mara baada ya mchezo kati yao na timu ya Yanga juzi usiku ambao ulimalizika kwa sare ya kutokufungana.

Shaaban alisema wakati wamejiandaa na mashindano hayo na wamedhamiria kuja kupambana kwa uwezo wao na mengine ambayo yatajitokeza hawatokuwa na mashaka nayo.

“Tunapambana kadri ya uwezo wetu lakini akitoka mchezaji kuchukuliwa na timu mwache apate riziki yake, lakini tukija hapa hatuji kwenye maonesho kwa sababu vijana wametoka Pemba wamekuja kupambana”, alisema.

Aidha alisema timu yao sio ngeni katika mashindano hayo na ni miaka miwili ndio ilifanya vibaya lakini mashindano mengi imekuwa ikifanya vizuri licha ya kutochukuwa ubingwa.

Alifahamisha kwamba timu yao imefanya mazoezi kwa muda wa wiki moja lakini anashukuru vijana wamefuata maelekezo na wamepambana.

Katika michuano ya mwaka jana Jamhuri ilipangwa kundi moja na Yanga na ilifungwa bao 1-0.