NA ABOUD MAHMOUD

UONGOZI wa timu ya soka ya Azam FC umekanusha uvumi ulioenea wa kutaka kumsajili mlinda mlango wa timu ya Jamhuri ya Pemba, Nassir Talib.

Akizungumza na Zanzibar Leo kwa njia ya simu, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam, Abdulkarim Amin ‘Popat’, alisema kauli hizo hazina ukweli kutokana na timu yake imeshasajili Mchezaji katika nafasi hiyo hivi karibuni.

Popat alisema Kocha Mkuu anaekinoa kikosi hicho alitaka wasijaliwe wachezaji wanne katika dirisha dogo ambapo mmoja wao ni mlinda mlango Mathias Kigonya na tayari wameshamtambulisha.

“Uvumi ulioenea mitaani kuwa tunataka kumsajili mlinda mlango wa Jamhuri hilo jambo sio kweli kwa sababu nafasi hiyo tayari imeshachukuliwa na Mganda Mathias Kigonya na wala hatuna mawazo ya kusajili watu wawili kwa nafasi moja,” alisema.

Aidha Mtendaji huyo alisema endapo watataka kuchukua mchezaji wa aina yoyote uongozi wake hautoshindwa kuwajulisha wapenzi na mashabiki wa klabu hiyo na soka kwa ujumla.

Hivyo aliwataka wapenzi wa Azam kuacha kusikiliza kauli zinazovuma mitaani na badala yake kusikiliza kauli za viongozi wa timu wanavyosema.

“Nawaomba wana Azam kuachana na kusikiliza kauli zinazozagaa mitaani kama jambo lipo kwetu hatutosita kusema kama tumemsajili au tunataka kumsajili mchezaji gani, hii ya mlinda mlango wa Jamhuri sio kweli na wala hatuna taarifa nazo,” alifahamisha.

Uvumi wa timu hiyo kutaka kumsajili mlinda mlango Nassir Talib umekuja baada ya kumalizika mechi kati ya Jamhuri na Yanga kwenye mashindano ya kombe la Mapinduzi ambapo ilidaiwa kuwa watu wawili waliojitambulisha kuwa wanatoka klabu ya Azam ambao waliomba namba za simu ya Nassir na kumwambia watamtafuta kuzungumzia ujio wake katika klabu hiyo ya Chamanzi jijini Dar es Salam.