Ataka jamii ichukie udhalilishaji wanawake, watoto

NA OTHMAN KHAMIS, OMPR

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla amewataka wazazi na walezi nchini kuwekeza katika sekta ya elimu ili jitihada hizo ziwe fursa na matunda bora yatakayowajengea maisha bira ya watoto wao.

Hemed alieleza hayo kwenye mahafali ya nane ya chuo cha ZanzibarShool of Healthy kilichopo Kwamchina Mwanzo, wilaya ya magharibi ‘B’ Unguja..

Katika mahafali hayo, makamu wa pili alitunuku stashahada katika fani za uuguzi na ukunga, ushauri nasihi, afisa tiba pamoja na astashahada ya ushauri nasihi, hafla iliyofanyika katika Uwanja wa Michezo wa Mao Zedong.

Alisema umefika wakati lazima wazazi lazima wabadilike na kujenga Utamaduni wa kutumia nguvu zao kubwa katika elimu ya kizazi chao badala ya baadhi yao kuendeleza tabia ya kutenga fedha nyingi kwa ajili ya kuwafanyia sherehe kubwa watoto wao wakati wanapofunga ndoa.

Alibainisha wazi kwamba katika karne hii ya sayansi na teknolojia elimu pekee ndio itakayowawezesha watoto kuingia katika ushindani na watoto wenzao ulimwenguni katika mfumo wa kujiamini kwenye soko la ajira.

Aliwapongeza wahitimu hao kwa kukamilisha mafunzo yao lakini wanalazimika kujipanga upya kwa kazi iliyo mbele yao juu ya namna watakavyolihudumia taifa katika misingi ya uaminifu na uadilifu kama walivyokula kiapo kwa wale wa kada ya uuguzi na ukunga.

Hata hivyo aliwaasa wahitimu hao kwamba wanaweza kuingia katika hatari ya kuachwa nyuma Kielimu baada ya miaka michache ijayo endapo hawatakuwa tayari kujielimisha Zaidi ili kwenda sambamba na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.

Aidha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza Uongozi wa Chuo hicho kwa kuanzisha fani ya madawa yaliyotanguliwa na yale ya kukabiliana na majanga ambayo wataalamu wake bado ni wachache hapa nchini.

Aliutaka Uongozi wa Chuo hicho kujipanga vyema katika muelekeo wa malengo yake ya kuelekea kuwa chuo kikuu na akaahidi kwamba serikali Kuu iko tayari kuunga mkono malengo hayo kwa vile yamejikita kuunga mkono jitihada za serikali kuu.

Alifahamisha kwamba kwa vile maafa yanapotokea hayana taarifa, lazima taifa lijipange kwa lengo la kuacha tabia ya kutegemea wafadhili au wataalamu wa kigeni pale yanapotokea.

Akigusia suala la udhalilishaji wa kijinsia unaowakumba zaidi wanawake na watoto wadogo, Makamu wa Pili alisema umefika wakati lazima Watu waache muhali kwa vile hakutapatikana hatia bila ya kuwepo ushahidi.

Alieleza kwamba kwa kuwa maisha ya watoto hivi sasa yako hatarini upo umuhimu wa kuanzishwa kwa mahakama maalum ya watuhumiwa wa Udhalilishaji ambao kwa sasa umekuwa ukihusisha pia baadhi ya Viongozi wenye dhamana kubwa katika Jamii.

“Inachafua kuona baadhi ya hata Mawakili katika maeneo yetu wamekuwa na tabia ya kuwatetea watu wanaohusika na vitendo vya udhalilishaji bila ya aibu wakijisahau kuwa wao ni miongoni mwa Jamii iliyowazunguuka,” alisema Hemed.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alionya kwamba Serikali Kuu itakapogundua  uwepo wa kiongozi anayejihusisha na tabia hiyo mbaya ya udhalilishaji  haitasita kumuwajibisha mara moja.

Mapema Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Chuo hicho, Ali Saleh alisema ndoto ya Zanzibar kuimarisha wa elimu inachipua kutokana na Sekta Binafsi kujitokeza katika kulea maeneo ya taaluma.

Saleh alieleza kwamba ipo nafasi kubwa ya ongezeko la ajira ya vijana kupitia Sekta Binafsi katika harakati zake za kushirikiana na Serikali katika kupambana na uhaba wa ajira  licha ya kwamba hivi sasa imeelemea zaidi katika masuala ya Utalii.

Akimkaribisha mgeni rasmi katika mahafali hayo, Waziri wa Eimu na Mafunzo ya  Amali Zanzibar, Simai Mohamed Said alisema kiapo walichokula wahitimu hao hasa wale wa fani ya uuguzi na ukunga kinapaswa kuwa dira ya kufanikisha wajibu wao katika kuhudumia wananchi.

Aidha Simai aliupongeza uongoziwa Chuo hicho kwa uharaka wake wa kuwafinyanga vijana unaokwenda sambamba na kasi ya sasa ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, awamu ya nane katika kuhudumia jamii.

Simai ambae pia ni kaimu Wazru wa Afya na Ustawi wa Jamii aliuthibitishia uongozi wa chuo hicho kwamba serikali itaangalia uwezekano wa kutafuta njia itakayopekea kupunguza kodi kwa sekta binafsi za taaluma.