NA OTHMAN KHAMIS, OMPR
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla jana ameshiriki kwenye mazishi ya marehemu Makame Ussi Ali, aliyewahi kuwa mkurugenzi wa Uhamiaji Zanzibar.
Mazishi ya mkurugenzi huyo yamefanyika jana huko kijijini kwake Kibuyuni Mkwajuni wilaya ya Kaskazini ‘A’, Mkoa wa Kaskazini Unguja, ambapo makamu wa Pili, aliungana na ndugu, jamaa na marafiki kwenye mazishi hayo.
Mzee Makame Ussi Ali aliyefariki nyumbani kwake mtaa wa Shaurimoyo mjini Zanzibar alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya kisukari kwa muda mrefu kabla ya mauti yake.
Akitoa salamu za rambi rambi na mkono wa pole akimuwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, Makamu wa Pili, alisema serikali inaungana na wafiwa hao katika msiba huo mzito na kuwataka wawe na moyo wa subra.
Hemed alisema mtihani wa msiba ulioikumba familia hiyo ni wa watu wote wakiwemo wapenzi na wangependa mzee Makame Ussi waendelee kuwa nae lakini Mwenyezi Mungu amemuhitaji kwa vile anampenda zaidi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa niaba ya Rais Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi aliwaomba wanafamilia hiyo wawe na subira katika kipindi hichi kigumu kwani bila shaka katika uhai wake mzee huyo alikuwa tegemeo kubwa kwao.
Mzee Makame Ussi Ali alipata elimu ya dunia sambamba na ile ya dini kama ada ya watoto wa mwambao iliyomuwezesha baadae kuingia katika kushika nyadhifa mbali mbali za utendaji na uongozi katika taasisi za serikali zote mbili ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Marehemu mzee Makame Ussi Ali ameacha kizuka mmoja na watoto watano, Mwenyezi Mungu ashushe rehema zake kwa kumnyooshea safari isiyo na shaka marehemu huyo.