NA OTHMAN KHAMIS, OMPR

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amesema hatua ya kutangazwa elimu bila malipo mara baada ya mapinduzi matukufu ya mwaka 1964, lengo lilikuwa kutanua fursa za elimu kwa wananchi wote.

Hemed alieleza hayo kwenye hafla ya ufunguzi wa skuli ya sekondari ya Donge Mkoa Kaskazini, ikiwa miongoni mwa shamrashamra za maadhimisho ya miaka 57 ya mapinduzi.

Alisema tangu serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilipotoa tangazo la elimu bure, wananchi wengi wamepata fursa ya kujipatia elimu na hivyo utaalamu wao walioupata umesaidia ujenzi wa nchi.

Alisema elimu bora ndio inayomuwezesha mwanaadamu hasa watoto wa taifa hili kukabiliana vyema na changamoto mbali mbali watakazokuwa wakipambana nazo katika maisha yao, wazazi na hata taifa kwa ujumla.

Hemed alieleza kwamba serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar awamu ya nane chini ya rais Dk. Hussein Ali Mwinyi itaendelea kutoa elimu bila ya malipo kwa taaluma ya msingi hadi sekondari ili kuwawezesha wanafunzi wenye sifa kupata elimu bila ya vikwazo.

“Rais wa Kwanza wa Zanzibar marehemu Mzee Abeid Amani Karume aliyeongoza Mapinduzi ya Zanzibar kwa lengo la kuwakomboa wazanzibari alitangaza elimu bure kwa wote bila ya ubaguzi wowote mnamo Septemba 23, 1964”, alisema Hemed.

Aliwapongeza wananchi wa Donge kwa jitihada, mshikamano, mashirikiano na ustahamilivu wao wa kuunga mkono jitihada za serikali katika kujiletea maendeleo hasa katika sekta muhimu ya elimu ambapo sasa jamii inashuhudia matunda hayo.

Hemed alifahamisha kwamba Donge ni mfano mzuri wa kuigwa na jamii nyengine hapa nchini kwa kujenga skuli kubwa na ya kisasa ya ghorofa jambo ambalo limesaidia kupunguza changamoto za ufinyu wa nafasi katika elimu ndani ya wilaya ya Kaskazini ‘B’.

Alisema ujenzi wa skuli hiyo ni kielelezo cha juhudi za serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuwaletea maendeleo wananchi wake ikiwa ni mkakati wa kuhakikisha nafasi za masomo kwa watoto wa visiwa vya Unguja na Pemba zinapatikana katika maeneo yote.