Ataka iwepo mikakati ya kukiuza kimataifa 

NA OTHMAN KHAMIS, OMPR

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amesema watanzania wanatakiwa kuongeza mikakati ya itakayohakikisha lugha ya kiswahili inaongeza watumiaji kwenye ghafla za rasmi za kimataifa.

Makamu huyo alieleza hayo jana mjini Dodoma katika ukumbi wa Hazina alipokuwa akifunga maadhimisho ya siku ya kiswahili, ambapo alisema inapaswa iwepo mikakati ya kuhakikisha lugha hiyo kubwa barani Afrika inapaa kimataifa.

Hemed alisema kiswahili ni bidhaa inayouzika kwenye soko la kimataifa na kuipatia manufaa makubwa nchi, hasa ikizingatiwa kuwa hivi sasa lugha hiyo imeanza rasmi kutumika katika mikutano inayoandaliwa na taasisi za kimataifa.

Alisema hadhi iliyofikia lugha hiyo hivi sasa imefungua milango kwa wataalamu wa kiswahili kufaidika kutokana na fursa zinazopatikana kwenye maeneo ya ukalimani, tafsiri, uandishi wa vitabu, uhariri na ufundishaji kwa wageni.

Alisema watanzania wenye uwezo wana fursa ya kushirikishwa wakati huu kwa kuanza kufungua vituo vya kufundishia lugha ya kiswahili na utamaduni katika mataifa yenye ofisi za balozi za Tanzania.

“Kiswahili ni miongoni mwa tunu za taifa letu na kimesaidia kutuunganisha na kutuwezesha kuwa wamoja na kudumisha mshikamano wa taifa, hivyo basi ni wajibu wetu kukiendeleza mahali popote tulipo”, alisema.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, alisisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha zaidi uchumi wa taifa unaokwenda sambamba na uuzaji wa bidhaa ya kiswahili ambayo mataifa mengine hushawishika kuipenda kutokana na kasi ya ukuwaji wa uchumi huo.

Alisema upo ushahidi kuwa mataifa mengi duniani ikiwemo Tanzania na Zanzibar kwa ujumla yamekufungua vituo vya kujifundishia lugha ya kichina kutokana na mataifa hayo kuwa na haja ya kufanya biashara na China.

Alieleza kwamba serikali zote Tanzania zinazingatia na kutilia mkazo suala la kukiendeleza kiswahili kwa kuzibaini na kuzitumia fursa mbali mbali za kiswahili zinazopatikana kutoka katika mataifa yenye watu wanaohitaji kujifunza lugha hiyo.

Kwa kuzingatia hayo alisema serikali hizo zitaendelea kubeba jukumu la kushirikiana na Baraza la Kiswahili la Taifa Tanzania (BAKITA) na Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA), wadau, taasisi na Idara za Kiswahili katika kuhakikisha watanzania wenye weledi wa kiswahili wanafaidika na lugha hiyo.

Hemed alimpongeza Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli kwa kutunukiwa nishani ya Shaaban Robert kutokana na mchango wake wa kukiendeleza kiswahili tangu alipoingia madarakani.

Awali akitoa taaifa ya uamuzi wa Baraza la Kiswahili Tanzania kumtunuku Tuzo ya Shaaban Robert Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli kutokana na msimamo wake wa kukiendeleza kiswahili, Mwenyekiti wa Bodi ya Baraza hilo, DK. Method Samuel alisema vigezo maalum vimewekwa ili kubaini mtu anayestahiki kupata nishati hiyo.

Dk. Samuel alifafanua kwamba ziara ya mwanzo ya Rais wa Jamuhuri yaMuungano wa Tanzania katika nchi za kusini mwa bara la Afrika mara baada ya kuchaguliwa Rais wa Tanzania, alijitahidi kukinadi kiswahili kitendo ambacho kimeleta mafanikio makubwa.

Akimkaribisha mgeni rasmi kuyafunga maadhimisho hayo ya siku ya kiswahili Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wa serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Abdalla Ulega alisema watanzania wana kila sababu ya kumshukuru Dk. John Pombe Magufuli kwa kuwa kinara wa kusimamia ukuaji wa lugha ya kiswahili.

Katika hafla hiyo ya ufungaji wa maadhimisho hayo ya siku ya kiswahili tuzo na vyeti mbali mbali vilitolewa kwa washirika wa lugha ya Kiswahili vikiwemo vyombo vya habari vya redio, televisheni na magazeti.