NA OTHMAN KHAMIS, OMPR

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amesema hatua ya kuendelezwa miradi inaijengea uwezo serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kutoa huduma bora za jamii kwa wananchi wote bila ya ubaguzi.

Makamu wa Pili alieleza hayo jana wakati alipomkaribisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi kuzungumza na wananchi kwenye kilele cha maadhimisho ya sherehe za mapinduzi.

Kilele cha sherehe hizo kilifanyika jana katika viwanja vya MnaziMmoja, ambapo Hemed alisema wananchi ndio wadau wakubwa wa kuvuna matunda ya mapinduzi kupitia miradi inayoanzishwa.

Hemed ambae pia ni mwenyekiti wa halmashauri ya sherehe na maadhimisho ya kitaifa, alisema sherehe za mapinduzi za mwaka 2021 zilijumuisha matukio 18 yaliyotanguliwa na usafi wa mazingira kwenye mikoa na wilaya mbalimbali za Zanzibar.

Alisema miradi tisa ya maendeleo ilizinduliwa kwenye shamrashamra za maadhimisho ya mapinduzi na miradi mitatu iliwekewa mawe ya msingi inayokisiwa kuwa na gharama za shilingi 46,179,920,020.

Hemed aliwahakikishia wananchi kwamba miradi hiyo mitatu iliyowekewa mawe ya msingi itamalizika kwa muda uliopangwa na kuonya kwamba serikali haitokuwa na muhali kwa watakaozorotesha kukamilika miradi hiyo.

Hemed alitoa shukrani kwa wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kwa kushiriki kikamilifu kwenye matukio mbali mbali ya sherehe za mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964 kutimia miaka 57.

Alifahamisha kwamba kujitokeza kwa wingi kwa wananchi hao kunaonyesha wazi wapo tayari na timamu kuendelea kuyalinda mapinduzi hayo yaliyolenga kumkomboa mwananchi wa Zanzibar kutokana na unyonge na madhila ya kutawaliwa.

“Wakati tunaadhimisha mapinduzi, tunawakumbuka wazee wetu waliopoteza maisha yao kwa kusimamia ukombozi, sasa hivi tupo huru tutaendelea kuwa huru kwa sababu mapinduzi daima na tutayalinda”, alisema.

Halkadhalika Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akiwa Mwenyekiti wa halmashauri ya sherehe na maadhimisho ya kitaifa aliwapongeza wajumbe wa kamati hiyo kwa maandalizi na usimamizi mzuri wa maadhimisho ya miaka 57 ya mapinduzi,

Pongezi kama hizo pia Hemed alizielekeza sambamba na kundi la wanahabari kwa kazi zao nzuri zilizofanikisha kwa kutoa habari kwa wananchi juu ya matukio yote ya sherehe hizo.