NA OTHMAN KHAMIS, OMPR

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amesema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefungua milango ya ushirikiano na sekta binafsi katika kuhakikisha fursa zilizopo zinachangia ukuaji wa uchumi.

Makamu huyo alieleza hayo jana alipokuwa akizungumza na Bodi ya Jumuiya ya Taifa ya Wafanyabiashara Zanzibar, huko ofisini kwake Vuga ambapo alisema sekta binafsi ndiyo muhimili wa uchumi, hivyo hakuna sababu ya kuwekwa nyuma kwenye ujenzi wa uchumi wa nchi.

Alisema yapo maeneo sekta binafsi inaweza kufanya vyema katika suala zima la kupunguza changamoto ya ajira, ambapo serikali inaweza kuingia kwa ajili ya uratibu hasa kwenye suala la uwekaji sera na sheria.

Hemed aliupongeza uongozi wa bodi hiyo kwa mtazamo wake wa kwenda sambamba na kasi ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya awamu ya nane jambo ambalo limeanza kuleta faraja hasa kitendo chao cha kuanza kwa utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa iliyoanza utekelezaji wake mwaka 2020/2050.

Aliitaka Bodi ya Jumuiya ya Wafanyabiashara Zanzibar kuangalia mapungufu yaliyomo ndani ya baadhi ya sheria zenye utata ili yaweze kufanyiwa marekebisho na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya washirika wa biashara.

Hemed aliwakumbusha viongozi wa bodi hiyo kuendelea na jukumu lao katika utoaji wa elimu juu ya umuhimu wa wafanyabiashara kulipa kodi jambo ambalo halina mjadala kwa vile ni wajibu wao kufanya hivyo.

Alisema wapo baadhi ya wafanyabiashara wenye tabia ya kupinda sheria zilizowekwa na badala yake kuendeleza dharau zinazojaa kiburi kinachopelekea wakati mwengine kutumia kisingizio cha majina ya viongozi ambao hawaelewi kama wanawachafulia heshima yao.

“Baadhi ya wafanyabiashara wanawachafulia viongozi na matokeo yake kusambaa mitandaoni kitendo ambacho Bodi ya Jumuiya ya Wafanyabiashara ina dhima ya kutoa taaluma kwa wafanyabiashara ili haki ya kulipa kodi ifanyike kwa vile haina mjadala”, alisema.

Akizungumzia suala la wataalamu wazawa, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema serikali iko kuwatumia wataalamu wake kwenye miradi mbali mbali ya kiuchumi na ustawi wa jamii.

Alisema tabia ya kuwadharau wataalamu wazalendo mbali ya kuwavunja moyo lakini pia inashindikana kuzitumia rasilmali zilizopo ikiwemo taaluma waliyopatiwa wataalamu hao inayotokana na nguvu kubwa iliyotolewa na serikali.

Mapema Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Jumuiya ya Kitaifa ya Wafanyabiashara Zanzibar, Ali Amour alisema sekta binafsi tayari imeweka mkazo wa kuhakikisha malengo yaliyokuwemo ndani ya Dira ya Taifa ya Mwaka 2020/2050 yanafikiwa.

Amour alisema katika kuunga mkono hatua hiyo muhimu kwa maendeleo na uchumi wa Taifa, Bodi imeamuwa kubadilisha mpango kazi wake wa miaka mitatu na kusogeza mbele miaka mitano ili kwenda sambamba na kasi ya serikali.

Nao baadhi ya wajumbe wa Bodi hiyo walimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba ajira 300,000 zilizoainishwa ndani ya ahadi ya serikali zitapatikana kama kutaandaliwa mazingira rafiki kwa sekta binafsi.

Walisema ushirikishwaji wa serikali za Mitaa katika maandalizi ya uanzishwaji wa miradi ya uwekezaji karibu na maeneo ya wananchi kwa kuwahamasisha wafanyabiashara kutumia fursa hizo kunaweza kuwa miongoni mwa njia za kuongeza nafasi ya ajira nchini.

Wajumbe wa Bodi hiyo walibainisha wazi kwamba maeneo mengine ya kilimo yaliyopo katika vijiji vya Kibuteni, Nganani na Mtule endapo yatajengewa mazingira bora ya miundombinu ya umeme na barabara hata zile za kifusi yanaweza pia kuwa chanzo cha fursa hizo za ajira.

Walishauri kuimarishwa kwa Chuo Kikuu cha Kilimo kilichopo Kizimbani ili kiwe na uwezo kamili wa vifaa vitakavyosaidia kutoa taaluma kwa wakulima hasa suala zima la utafiti wa udongo unaohitaji matumizi sahihi ili kujua kilimo gani kinachopaswa kuendelezwa.