NA OTHMAN KHAMIS, OMPR

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amevutiwa na utayari uliooneshwa na viongozi wa vyama siasa wa kuwa tayari kushirikiana na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuwatumikia kwa kuwaletea maendeleo wananchi.

Hemed alieleza hayo jana huko ofisini kwake Vuga jijini Zanzibar alipokuwa akizungumza na viongozi wa vyama tisa vya siasa vilivyopo hapa nchini, ambapo baadhi yao walisimama kwenye kinyang’anyiro cha urais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 28 mwaka jana.

Viongozi walikwenda ofisini kwa Makamu wa Pili wa Rais kwa madhumuni ya kuipongeza serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya awamu ya nane kutokana na kuanza kazi zake kwa kasi kubwa sambamba na kueleza utayari wao wa kuiunga mkono.

Makamu huyo alisema amefurahishwa na viongozi hao kwa utayari wao wa kushirikiana na serikali ya mapinduzi ya Zanzibar na kueleza kuwa serikali nayo iko tayari kushirikiana nao kwa wakati wowote kwa ajili ya kuendeleza ustawi wa maisha ya wananchi.

Alisema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya awamu ya nane imeundwa chini ya mfumo wa Umoja wa Kitaifa (GNU), uliotokana na misingi ya maridhiano kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Makamu alisema mchango na mawazo ya viongozi wa vyama vya kisiasa una umuhimu mkubwa katika kujenga nchi na hivyo hauna mjadala kwani mawazo yao yanalenga kutoa fursa pana zaidi ya kuimarisha umoja, mshikamano na kukuza maendeleo kwa wananchi.

Aliwathibitishia viongozi hao wa kisiasa kwamba serikali itaendelea kutoa ushirikiano wakati wowote katika kuhakikisha kwamba huduma za jamii zinawafikia watu wote na pale inapotokea athari ndani ya utekelezaji huo isipuuzwe na ni vyema ikaripotiwa panapohusika.

Akizungumzia suala la amani na utulivu nchini, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, alisema mchango wa viongozi wa kisiasa ni muhimu katika kusimamia hali ya umoja, usalama na amani ya nchi.

“Kuna kila sababu kwa viongozi wa vyama vya kisiasa kuendelea kusimamia suala la amani na utulivu kutokana na kuwa na sauti na mvuto wa kukubalika na jamii inayowazunguka”, alisema Hemed.

Aliwapongeza viongozi hao kwa kuingia kwenye mchakato wa uchaguzi mkuu kwani kwa kufanya hivyo kulidhihirisha uwepo wa demokrasia visiwani hasa ikizingatiwa kuwa walipewa uhuru wa kutosha wa kunadi sera zao bila ya kubanwa wala kubughudhiwa.

Alifahamisha kwamba maisha baada ya uchaguzi yanaendelea ni vyema kila mwananchi akaendelea kutekeleza wajibu wake huku akiwataka wawe na subra katika kipindi hichi ambacho Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi akichukua maamuzi magumu yatakayosaidia kujenga nchi.

Awali viongozi hao walisema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefanya jambo kubwa kwa kuendelea kutumia mfumo wa Umoja wa Kitaifa utakaosaidia wananchi kuendeleza misingi ya ushirikiano na mshikamano.

Walisema uhasama unaotokea kabla na baada ya uchaguzi umefifia katika kipindi kifupi kutokana na maono ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya awamu ya nane.