NA OTHMAN KHAMIS, OMPR

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, amesema watendaji wa Idara ya Ustawi wa Jamii wana jukumu la kusimamia matunzo ya wazee katika nyumba za Welezo na Sebleni.

Hemed alieleza hayo jana wakati alipozungumza na viongozi, wafanyakazi na wazee wanaotunzwa nyumba za Sebleni na Welezo, wakati alipofanya ziara maalum katika nyumba hizo kuangalia mazingira ya makaazi ya wazee hao na kufahamu changamoto zinazowakabili.

Makamu alisema pale zinapoibuka changamoto ndogo ni vyema kwa watendaji kushirikiana na viongozi waziwasilishe katika ngazi husika bila ya kuvunjika moyo ili malengo ya serikali ya kuwapatia huduma za makaazi wazee wasiojiweza yalete mafanikio.

Hemed alitahadharisha kwamba hakuna mzee hata mmoja anayeweza kulalamika bila ya kuwepo sababu, hivyo kinachohitajika ni kuhakikisha busara zaidi zinatumika katika kuwapatia huduma stahiki wazee hao ili waendelee kuishi kwa amani na upendo.

Alibainisha kwamba wazee lazima wahudumiwe ipasavyo kutokana na hali halisi ya mazingira yao kiumri na kiafya ambapo hawastahiki kukaa na njaa muda mrefu.

Makamu wa Pili aliutaka uongozi wa wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto kuandaa utaratibu kila mwezi utakaowapatia huduma za afya wazee hao.

“Iwe mwiko kwa mzee mwenye umri mkubwa kukaa foleni ya kumuona daktari kwa ajili ya kupata huduma za afya, kwa umri wao wanahitaji kutunzwa katika mazingira bora”, alisema Hemed.

Alisema haipendezi na ni jambo la masikitiko kumuona mzee mwenye umri mkubwa anapanga mstari wakati anapohitaji huduma za afya hospitalini.

Awali wazee wanaotunzwa katika nyumba za Sebleni na Welezo, waliipongeza serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa hatua inazoendelea kuzichukua za kuwahifadhi na kuwapatia huduma.