NA ABDULKARIM KHAMIS
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, amesema Zanzibar inahitaji wataalamu wazalendo kwenye fani mbalimbali ambao mchango wao utasaidia kuharakisha maendeleo ya nchi.
Makamu huyo alieleza hayo jana huko ofisini kwake Vuga mjini Zanzibar, wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.
Alisema moja ya sababu iliyochangia mataifa makubwa kupiga hatua kubwa za kiuchumi na kimaendeleo ni kusomesha wananchi wao na kupata wasomi uliofanikisha maendeleo hayo.
Hemed alisema serikali inathamini mchango wa vyuo vya elimu ya juu vilivyopo nchini kikiwemo Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, ambacho kinaendelea kutoa wataalamu wa fani mbalimbali.
Aidha Makamu aliupongeza uongozi wa chuo hicho kutokana na uamuzi wa kuanzisha kampasi yake kisiwani Pemba na kueleza kuwa hatua hiyo muhimu itasaidia zaidi wananchi na hasa vijana wa Zanzibar kuendelea kupata taaluma kwa urahisi.
Alieleza mafanikio yaliyopatikana katika chuo hicho yanatokana na mashirikiano ya kina na ameuhakikishia uongozi huo kwamba serikali itaendelea kuwaunga mkono.
Alibainisha kwamba kwa vile watanzania wanaendelea kufaidi matunda ya chuo hicho, ipo haja ya kutanua wigo wa elimu nchini, kwani wahitimu wa taasisi hiyo tayari wanatumika katika sekta mbali mbali za serikali na hata zile binafsi.
Hemed alielezea faraja yake kutokana na kasi ya taasisi hiyo ya elimu inayokwenda sambamba na utayari wa awamu ya nane wa kuleta maendeleo kwa wananchi ikiwategemea zaidi wasomi hao.
Kwa upande wake mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Prof. Shadrack Mwakalila alisema wanafunzi na wahadhiri wa chuo hicho wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa dakhalia.
Katika kukabiliana na tatizo hilo linalochangia kupunguza muda wa masomo Prof. Mwakalila alieleza kwamba uongozi wa chuo umeandaa utaratibu wa kuanza ujenzi wa majengo ya dakhalia yatakayotoa huduma kwa wanafunzi 1,960.
Aidha Pro. Mwakalila alieleza kuwa licha ya kuwapa elimu wanafunzi chuoni hapo, pia wanawajenga kuwa na uelewa wa uongozi na maadili, pamoja na mbinu za kujua namna bora ya kujiajiri ili kuondokana na dhana ya kusubiri ajira serikalini.
Kwa kutambua uwajibikaji wa serikali ya awamu ya nane inayoongozwa na Dk. Hussein Ali Mwinyi, Prof. Mwakalila alimpongeza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman kwa utendaji wake ambao unaleta matumaini makubwa kwa watanzania.
Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Kampasi ya Karume Zanzibar kilianza na wanafunzi 22 mwaka 2013, ambapo hadi kufikia 2020 kina jumla ya wanafunzi 1,920.