Ni ugonjwa unaoongoza kuwashambulia watoto wengi Zanzibar
Ni wale waliochini ya umri wa miaka mitano
NA MOHAMMED SHARKSY, (SUZA)
UGONJWA wa pneumonia (homa ya mapafu) unaonekana kuwa ni tatizo kubwa hasa kwa watoto waliochini ya miaka mitano.
Zanzibar kama sehemu ya dunia nayo kwa kiasi kikubwa huathiri afya ya wazanziibari huku kundi kubwa likiwa la watoto ukilinganisha na watu wazima.
Katika Makala hii ya afya tunazungumzia kuhusiana na hali halisi ya ugonjwa wa homa ya mapafu Zanzibar, ikiwa ni pamoja na dalili, tiba na kinga ya ugonjwa huo.
Kimsingi mwili wa binadamu una mapafu mawili yenye maumbile yanayofanana ambapo kazi kuu ya mapafu ni sehemu ya mwili inayoingiza oksijeni mwilini na kuipeleka kwenye seli za mwili. Ni kiungo muhimuj na kikuu kwenye mfumo wa upumuaji.
Inapotokea mtu au mtoto kupata homa ya mapafu, vifuko hivi hujaa maji au usaha, hivyo huathiri upitishaji wa hewa safi kwenye damu na kusababisha tatizo la kupumua.
Homa ya mapafu au ‘pneumonia’ ni ugonjwa unaoshambulia mfumo mzima wa hewa, ni aina ya maambukizi yanayoathiri mapafu. Aidha ni ugonjwa unaoua watoto wengi hasa katika nchi zinazoendelea duniani ikiwemo Zanzibar. Inakadiriwa kwamba watoto karibu milioni 1.6 walio chini ya miaka mitano wanakufa kila mwaka kutokana na ugonjwa huu.
Akizungumza na Makala haya, Nasra Sleyyum Ali, Dakatari bingwa wa watoto katika hospitali kuu ya Mnazi Mmoja, alisema kuwa kuanzia Januari 1 hadi jana jumla ya watoto 68 wameripotiwa kuugua ugonjwa huo.
Alisema watoto hao ni wale tu waliofikishwa hospitalini hapo na kulazwa mbali na hospitali za mashamba na vituo vya afya vya hapa Unguja.
“Hizi ni kesi za watoto waliolazwa Mnazimmoja tu inawezekana wakawepo wengi Zaidi ya hao “, alisema.
Akieelezea hali halisi ya ugonjwa huo hapa Unguja, Daktari Nasra, alisema ugonjwa huu unashika nafasi ya kwanza kati ya magonjwa ynayowasumbua watoto kiasi kwamba wakati mwengine hulazimika kulazwa kitanda kimoja watoto wawili.
Alitaja maeneo wanaotoka wagonjwa hao kuwa ni pamoja na Wilaya zote za Magharibi Unguja ikifuatiwa na wilaya ya Mjini.
Nae Sabra Salum Suleiman Muuguzi, Mkuu wa hopital ya Wete Pemba aliiambia gazeti hili kwamba katika mwaka uliopita 2020 kuanzia Januari mpaka Disemba jumla ya watoto 1,022 wamelazwa kwa maradhi mbali mbali katika hospitali hiyo.
Aliyataja maradhi hayo kuwa ni pamoja na homa ya mapafu watoto 280 ugonjwa ambao unaongoza kwa watoto waliochini ya umri wa miaka mitano.
Muuguzi huyo aliwataja kati ya watoto hao wanaume ni 151 na wanawake 119 ambapo kwa mwaka 2019 watoto waliolazwa walikuwa ni 1,431, kati yao 389 waliuguwa homa ya mapafu na saba kati yao walifariki dunia.
Alisema kuwa hizo ni takwimu za hospitali kwa wagonjwa waliolazwa na kupata matibabu katika hospitali ya Wete pekee.
VIHATARISHI VYA HOMA YA MAPAFU
Miongoni mwa vihatarishi vya homa ya mapafu kwa watoto ni ukosefu wa kinga mwilini, ukosefu wa lishe bora hasa kwa watoto wachanga ambao hawanyonyeshwi ipasavyo.
Aidha mazingira duni ya makaazi hasa yenye moshi wa sigara au moshi wa kuni wa ndani ya nyumba ni moja inayosababisha vihatarishi vya homa ya mapafu hasa kwa watoto.
Msongamano ndani ya nyumba kutokana na watu kuwa wengi sehemu moja kwa kiasi kubwa inachangia watoto kupata homa ya mapafu.
SABABU ZA UGONJWA WA HOMA YA MAPAFU
Homa ya mapafu inasababishwa na vimelea vya maradhi kama vile bakteria, virusi, parasiti na fangasi.
Kwa kawaida vimelea hushambulia mwili wa binadamu kulingana na umri na kinga ya mwili. Kwa mfano, bakteria wanaosababisha homa ya mapafu kwa watoto wachanga ni tofauti na wale wanaosababisha ugonjwa huo kwa watoto wakubwa.
Baadhi ya vimelea wa bakteria wanaoshambulia watoto ni pamoja na ‘streptococcus pneumoniae’ ambao ni aina ya bakteria wanaoongoza kusababisha homa ya mapafu kwa watoto katika visiwa vyetu.
Wapo pia ‘haemophilus influenzae’ aina b (HIB) ambao ni aina ya pili ya bacteria walio maarufu zaidi kwa kusababisha ugonjwa wa homa mapafu kwa watoto.
‘Staphylococcus aureus’ ni aina nyingine ya bacteria ambao hushambulia zaidi watoto wachanga. Kuna pia kundi B streptococci, ambao pia hushambulia zaidi watoto wachanga.
Kwa upande wa virusi, virusi wa aina ya ‘respiratory syncytial virus’, ndiyo wanaoongoza kwa kusababisha homa ya mapafu kwa watoto.
Aidha, vimelea wa ‘pneumocystis jiroveci’ ambao kwa sasa huwekwa kwenye kundi la parasiti ni maarufu zaidi miongoni mwa parasiti wanaosababisha homa ya mapafu kwa watoto wenye upungufu wa kinga mwilini hususani watoto wenye VVU.
Aina nyingine za bakteria ambao hushambulia zaidi watoto wakubwa ni pamoja na ‘mycoplasma pneumonia’ na ‘chlamydia pneumonia’.
JINSI HOMA YA MAPAFU INAVYOATHIRI WAGONJWA
Mara nyingi inapotokea kinga ya mwili ya mtoto imeshuka kwa sababu yeyote ile, vimelea hivi huweza kusambaa na kufika mpaka sehemu ya chini ya mfumo wa njia ya upumuaji (lower respiratory tract) na hatimaye kushambulia mapafu.
Halkadhalika, vimelea hawa wanaweza kuenea kwa njia ya damu kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kabla ya kuzaliwa, yaani kipindi cha ujauzito
DALILI ZA UGONJWA WA HOMA YA MAPAFU
Kwa watoto wadogo, dalili za awali zinaweza kuwa homa kali pamoja na mtoto kuhangaika, kunyong’onyea kung’ang’anaa. Watoto wanaozaliwa wakiwa na uambukizi wa vimelea aina ya ‘streptococcus’ kundi ‘B’ ambao wanasababisha anaeugua kupumua kwa shida.
Wakati mwingine mtoto anaweza kuwa na dalili ambazo si maalum kama vile kuhangaika na kushindwa kunyonya au kula vizuri bila kuwa na dalili yeyote ya kushindwa kupumua.
Kulia sana kwa mtoto hali hii inaweza kutokea kwa mtoto wa umri wowote ule.
Dalili nyengine za homa ya mapafu ni homa kali, kuhisi baridi, kikohozi, kupumua kwa haraka kuliko kawaida, kutoa sauti isiyo ya kawaida wakati wa kupumua, mbavu za mtoto kuingia ndani wakati wa kupumua na maumivu ya tumbo.
Aidha dalili nyengine ni kupoteza hamu ya kucheza, kupoteza hamu ya kula mtoto kubadilika rangi na kuwa na rangi buluu katika midomo na kucha
Hata hivyo, si lazima dalili zote hizi ziwepo kwa kila mtoto. Baadhi ya watoto huonesha kupumua kwa haraka kama dalili pekee ya homa ya mapafu.
Iwapo vimelea vimeshambulia sehemu za chini ya mapafu karibu ya tumbo, sehemu ijulikanayo kama kiwambo au ‘diaphragm’, mtoto anaweza asioneshe hali yeyote ya kushindwa kupumua ingawa anaweza kuwa na homa na kujihisi maumivu makali ya tumbo, vichomi na pia kutapika.
Kwa watoto wachanga zaidi wanaweza kushindwa kunyonya na pia kupoteza fahamu na kupata degedege.
UCHUNGUZI NA VIPIMO
Daktari humchunguza mtoto kwa kusikiliza dalili za ugonjwa kutoka kwa kutumia kipimo kinachoitwa ‘stethoscope’.
Vipimo hivyo ni pamoja na X-ray ya kifua, au CT-scan ya kifua, pamoja na damu ili kuchunguza madhara yaliyoletwa na homa hii ya mapafu.
X-ray ya kifua na CT-scan ya kifua vina uwezo wa kuonesha tatizo hata pale ambapo daktari ameshindwa kusikia sauti maalum kwa kutumia kifaa chake cha ‘stethoscope’.
MATIBABU
Matibabu homa ya mapafu hutegemea ni aina gani ya vimelea ya maradhi, umri na hali ya yule mtoto ilivyo.
Mara nyingi dawa za maji za ‘antibiotics’ kama vile ‘erythromycin’, ‘benzylpenicillin’, ‘cefotaxime’, ‘amoxycillin’, ‘clarithromycin’ na kadhalika hutumika kutibu homa na maambukizi huku dawa za panadoli na ‘ibumex’ hutumika kushusha homa ya mwili.
Ikumbukwe kwamba dawa za ‘antibiotics’ hazina uwezo wowote wa kutibu homa inayosababishwa na virusi (viruses), kwa hiyo hupona kwa kutumia tu dawa za kushusha homa, lishe, mazingira yenye hewa safi na kumpa mtoto maji mengi.
Na hii ieleweke kwambaa ni daktari pekee ndiye anayeweza kufahamu kama mtoto anahitaji ‘antibiotics’ au dawa za aina nyingine. Kwa hiyo ni muhimu kwa mzazi ama mlezi kumpeleka mtoto kituo cha afya au hospitalini haraka pindi anapoonesha dalili za ugonjwa badala ya kuamua kumpa dawa bila kufuata ushauri wa wataalamu wa afya.
KINGA HOMA YA MAPAFU
Homa ya mapafu inaweza kuzuiliwa kwa chanjo, chanjo dhidi ya Hib, pneumococcus, surua na kifaduro ni njia mojawapo ya kuzuia homa ya mapafu.
Mtoto kuishi katika mazingira yenye hewa safi.
Lishe ya kutosha ni muhimu kwa kuboresha kinga ya mwili ya mtoto ambapo inashauriwa mama kunyonyesha mtoto bila kuchanganya na kitu chochote walau kwa miezi sita ya mwanzo ya maisha yake.
Kuweka usafi katika makaazi kama kutotumia jiko la mkaa au kuni ndani ya nyumba na uvutaji wa sigara ni jambo linaloshauriwa pia.
INDHARI
Tafiti nyingi duniani zimeonyesha kwamba kinga na tiba sahihi ya homa ya mapafu inaweza kuzuia vifo milioni 1 kwa watoto duniani kila mwaka. Hivyo ni wajibu wetu sote kushirikiana kupambana na ugonjwa huu.