LONDON, England
MSHAMBULIAJI wa zamani wa kimataifa wa Nigeria, Odion Ighalo yuko wazi kuhamia Marekani huku akiangalia uhamisho kwenda klabu ya Ligi Kuu ya MLS ya Inter Miami.


Nyota huyo mwenye umri wa miaka 31 yuko mbioni kurudi katika klabu yake ya Shanghai Greenland Shenhua kufuatia miezi 12 ya mkopo kwa miamba ya England ya Manchester United.


Ighalo atarudi Shenhua inayoshiriki Ligi Kuu ya China mwishoni mwa mwezi, lakini, hajapanga kubakia China kwa muda mrefu.
“Nimekuwa nikitazama MLS na ligi inafanya vizuri na ningependa kucheza kwenye MLS,” Ighalo aliiambia ESPN.


“Lazima nisubiri ofa na ikiwa nafasi itajitokeza, nitaichukua kwa sababu ligi inafanya vizuri na ni maisha mazuri na ningelipenda hili.
“Wachezaji wengi huenda huko. Hata Gonzalo Higuain kutoka Juventus yupo, pia Giovanni dos Santos. Kwa nini isiwe hivyo? Ningependa kwenda huko ikiwa fursa itatokea”, aliongeza.


“Kuwa mchezaji mzoefu, kwenda huko, kufanya vizuri. Ni fursa ikiwa inakuja kwangu. Klabu ya David Beckham [Inter Miami] inakua, kwa hivyo ikiwa nafasi inatokea kwanini sivyo?”.
Ighalo alivutiwa kama mchezaji mzuri katika raundi ya pili ya msimu wa 2019/20 akifunga mara tano kutoka kwenye mechi 19 za ushindani akiwa United.


Mchezaji huyo wa zamani wa Watford amejitahidi kucheza msimu huu akiwa amecheza mara nne tu, lakini, hajutii kujiunga na ‘mashetani wekundu’.
“Ilikuwa nzuri na ngumu, kabla ya kuja United sikuwahi kufikiria nitacheza,” alisema. Mimi ni shabiki wa ‘wekundu’ hao. Ukimuuliza mtu yeyote nilikulia, tunapigana kwa sababu ya Manchester United”, alisema.


“Tunagombana na kubishana. Kwa hivyo wakati timu yangu haikufanya vizuri wangeanza kunitukana na kubishana nami na nililia. Ninaweza kukuambia mimi ndiye mtu mwenye furaha zaidi duniani kwa ndoto yangu kutimia, nimetimiza ndoto yangu.


“Nakumbuka usiku wakala wangu alinipigia simu kuniambia Manchester United inanitaka, ilikuwa saa 10 au 11 jioni wakati wa Shanghai. Nilikuwa chini ya kitanda changu, sikulala mpaka alfajiri”, aliongeza.


“Sijali kupunguziwa mshahara, nataka tu kwenda Manchester United kwa sababu hii ni ndoto yangu. Nilikuwa chini ya kitanda changu nikitetemeka na nikitembea kuzunguka chumba changu na sikulala hadi saa 6 asubuhi.
“Nimetimiza kama mchezaji wa mpira, ikiwa sitafanikiwa chochote kutoka sasa wakati ninapomaliza taaluma yangu nimetimiza.”
Ighalo ambaye alifunga magoli 16 kutokana na mechi 35 za kimataifa akiwa na Nigeria, ana kandarasi ya Shenhua hadi 2024.(Goal).