ZASPOTI
Awafundisha warembo mitindo tofauti ya Hijab
WANAMITINDO wa kimataifa wanahamasisha mamilioni ya wasichana kuiga muonekano wa staili zao ikiwemo mitindo ya nguo, nywele, muonekano wa maumbile yao, ambapo hupelekea hadi baadhi ya watu kufikia kufanya operesheni ili tu wafanane na mwanamitindo fulani.
Imezoeleka kuwa moja ya sifa ya mitindo ya kimataifa ni kupiga picha na mavazi yanayoonesha maumbile yao (nusu uchi), ambayo hupelekea kuvutia wengi na kupata pongezi kutoka sehemu nyingi ulimwenguni.
Jambo hilo liliwanyima fursa na kuwa ni mwanzo kwa wasichana wengi wa kiislamu wenye ndoto za kuwa wanamitindo wa kimataifa kwa kuheshimu tamaduni za dini zao.
Kama mwanamke wa kiiislamu, Ikram Abdi Omar, ameweza kuwa mwanamitindo wa kimataifa aliyeweza kufanya kazi hiyo akiwa na hijabu kichwani, ambae alikuwa ni wa kwanza nchini Uingereza kuvaa hijabu kwenye jarida mashuhuri la Vogue na hata kufanya kazi na kampuni maarufu ulimwenguni ya Burberry mnamo mwaka 2019.
Kuwa mwanamitindo wa kimataifa ambae unajistiri maungo na hata kuvaa hijabu kichwani ni jambo kubwa la uthubutu ambalo linapelekea kubadilisha tasnia ya urembo na mitindo na kushajihisha wanawake wengi kutoka kwenye jamii ya kiislamu wenye ndoto hiyo.
Uthubutu wa mwanamitindo huyo ulinisukuma kuingia ndani zaidi ili kujua historia yake.
Ikram Abdi Omar (24) ni Msomali aliyezaliwa Sweden, ambae kwa sasa anaishi Bristol, ni msichana mwenye vipaji vingi, ambae alisoma shahada yake ya kwanza ya sayansi ya tiba katika Chuo Kikuu cha Bristol.
Wakati Ikram akiwa bado anasoma katika Chuo Kikuu hicho, alianza kupata umaarufu ambapo alisainiwa kuingia kwenye tasnia hiyo na Waziri Mkuu wa Usimamizi wa Mitindo mnamo mwaka 2018.
Kabla ya kutambulika kwake ulimwenguni kupitia onyesho la ‘Molly GoddardFW18’ mwanamitindo huyo wa Somalia alishiriki katika onesho la mitindo huko London liitwalo ‘Modest Fashion Week’.
Pia alipata umaarufu katika kampeni ya kuogelea ya Nike na akaweka historia ya mitindo wakati alipoonekana kwenye jarida la Vogue Arabia na wanamitindo wenzake waliovaa hijabu, Halima na Amina Aden ambao walikua wa kwanza kwa Vogue kuleta utofauti mkubwa kwa kuvaa hijabu.
Pia alipata umaarufu katika kampeni ya kuogelea ya Nike na akaweka historia ya mitindo wakati alipoonekana kwenye jarida la Vogue Arabia na wanamitindo wenzake waliovaa hijabu, Halima na Amina Aden ambao walikua wa kwanza kwa Vogue kuleta utofauti mkubwa kwa kuvaa hijabu.
Akizungumzia uthubutu wake wa kuingia kwenye mitindo ya kimataifa akiwa na hijabu, Ikram, alisema, urithi na imani yake ya kidini imeleta hamasa na utofauti mkubwa katika tasnia hiyo ya mitindo.
“Ninaamini jukumu langu katika tasnia hii linajumuisha uwezeshaji na uhamasishaji wa wanawake wa jamii yangu wenye ndoto hii, kwa sababu imeanza kukubalika kuwa wanawake kwenye tasnia ya mitindo, wana chaguo la kuvaa vile wanavyopenda, iwe ni pamoja na kuonyesha ngozi au la” alisema.
Ikram, alisema, anaelewa kuwa ni ngumu kwa wasiokuwa waislamu kuelewa umuhimu wa kuvaa hijabu, hivyo alieleza kuwa hijabu yenyewe ni jambo la maana, kwani inamaanisha kuwa ni unyenyekevu kwa dini yake na huonesha ukaribu na mungu wake.
“Ni chaguo langu binafsi kuvaa kutokana na madhehebu ya dini yangu na inategemea jinsi unataka wewe mwenyewe kuvaa hijabu, kwani hiki ni kipimo jinsi gani uko karibu na Mungu au dini yako pia”, anaeleza.
Pia, alisema, kuvaa hijabu katika mitindo inaonyesha ujasiri na ni ukumbusho kwamba ana chaguo la kuvaa jinsi anatakavyo na ni uthibitisho kuwa unaweza kufanya kazi hiyo bila ya kujitolea imani yako.
Mwanamitindo huyo mwenye asili ya Somalia, wakati akiwa na umri wa miaka minane, alihamia Bristol pamoja na wazazi wake ambapo alianza kuvaa hijabu akiwa na umri wa miaka 11.
Kupitia uvaaji wake wa hijabu, Ikram amejua sanaa ya uratibu wa rangi na mavazi, “Kwa kweli siwezi kuhesabu nina hijabu ngapi , kiufupi nnazo aina nyingi na kila wakati ninapokuwa na hafla mimi hununua mpya, kwa sababu sio ghali na kila wakati ninataka niwe na muonekano mpya.
Kila wakati amekuwa akipenda kujaribu kutafuta njia mpya za kutengeneza kitambaa cha kichwa kuendana na nguo zake, ambapo mtindo wake unabadilika kila wakati kwani anapenda kujionyesha kwa njia tofauti, ambapo alieleza kuwa jambo muhimu juu ya mitindo ni kujaribu.
Ikram alikua na ndoto ya kuwa mwanamitindo tangia akiwa mtoto, ambapo aliutumia muda wake wa kucheza kwa kubadilisha mavazi na kutembea mbele ya marafiki zake akiigiza wanamitindo wakubwa wa kipindi hicho.
Mlimbwende huyo ana matumaini makubwa ya kubadilika kwa tasnia ya mitindo ulimwenguni ambapo kupitia yeye na wenziwe wachache walioanza kuvaa hijabu kwenye mitindo ya kimataifa yataleta taswira mpya kwa wanaopenda stara.
Alisema kupitia yeye wasichana watapata uthubutu wa kutimiza ndoto zao na hata kwa wasiokuwa waisilamu watatumia hijabu kama moja ya fasheni mpya kwao.
Mlimbwende huyo pia ameanzisha kituo chake cha ‘YouTube’ ambapo hutuma video ambazo zinaonyesha namna ya kujiweka mrembo kutumia ‘make up’ na kufundisha mitindo tofauti ya kufunga hijabu.
“Ninapenda kuona wasichana wengine wanaiga mitindo yangu kadhaa na waone kuwa mitindo na mavazi ya wanamitindo wakubwa, kuwa anaweza kuvaa hata msichana wa kawaida katika hafla tofauti”, alisema.
Ingawa imechukua muda mrefu kufika hapa, lakini, tasnia ya mitindo inaonekana hatimaye imekubali wazo la kuwa na wanamitindo wenye kuvaa hijabu.
Matumaini yake ni kuwa tasnia ya mitindo ulimwenguni hususani ya kimataifa itakuwa na warembo wengi wa kiislamu ambao watatumia tamaduni zao bila kuzificha ili kuubadilisha mtazamo wa mitindo duniani.
“Ikiwa wewe ni mwanamitindo ambaye huvaa hijab, ni hatua ya ujasiri mbele ya ambao wanataka kuingia kwenye tasnia na kutembea kwenye steji la kuonesha aina mbali mbali za mitindo wakiwa na mavazi ya stara pamoja na hijabu” Ikram.