USWIZI, GENEVA

SHIRIKA la Kazi la Kimataifa ILO, linakadiria kwamba asilimia 8.8 ya saa za kazi duniani ilipotea mwaka wote wa 2020, ikilinganishwa na robo ya nne ya mwaka uliotangulia.

Shirika hilo la UN lenye makaazi yake mjini Geneva nchini Uswizi lilitoa makadirio ya hivi karibuni .

Limetoa makadirio hayo kila baada ya miezi mitatu, likiyalinganisha na kipindi cha mwezi Oktoba hadi Disemba mwaka 2019 ambapo janga la virusi vya korona lilikuwa bado halijaanza kusambaa kote duniani.

Shirika hilo limesema kupotea kwa asilimia 8.8 kulikuwa sawa na ajira za kudumu milioni 255. Hii ilikuwa idadi kubwa mara nne zaidi ya idadi iliyopotea wakati wa mdororo wa kifedha duniani mwaka 2009.

Aidha shirika hilo linatabiri kwamba nchi nyingi zitashuhudia uimarikaji wa hali hiyo katika nusu ya pili ya mwaka wa 2021 wakati mipango ya utoaji chanjo ikitekelezwa.

Lakini chini ya makadirio yake ya msingi, kupotea kwa asilimia 3 ya saa za kazi duniani kunakadiriwa mwaka wa 2021, ikilinganishwa na robo ya nne ya mwaka 2019.

ILO inatoa wito wa kuwepo kwa hatua mahususi za kuwasaidia wanawake, vijana na makundi mengine yaliyoathiriwa zaidi na janga hilo.