NA ABOUD MAHMOUD
MASHIRIKIANO baina ya Zanzibar na India ni njia sahihi iliyosaidia kuinua uchumi katika nchi mbili hizo kupitia sekta mbali mbali.
Balozi mdogo wa India anaefanya kazi zake visiwani humu, Bhagwant Singh, alieleza hayo wakati wa maadhimisho ya miaka 72 ya uhuru wa India yaliyofanyika katika ofisi za ubalozi huo juzi.
Balozi Singh alieleza kuwa mashirikiano kati ya pande mbili hizo yamesaidia kuinua uchumi wa nchi hizo, kuimarisha elimu na biashara jambo linalopaswa kuendelezwa.
“India na Zanzibar ni ndugu wa muda mrefu ambao tumeweza kusaidia nchi zetu mbili hizi kuziinua kiuchumi kupitia sekta ya elimu na biashara,” alisema.
Aidha alisema kupitia siku ya uhuru wa India wananchi wake hawana budi kuyaendeleza mashirikiano hayo ambayo yataleta maendeleo zaidi kupitia sekta mbali mbali za kiuchumi na kijamii.
Balozi huyo pia alisema nchi yake imefanikiwa kujifunza mambo mengi kutoka Zanzibar ikiwemo kujenga heshima ya mataifa mbali mbali kuishi katika nchi yake bila ya kubughudhiwa.
Alisema kutokana na hilo India itaendelea kupigania kuendeleza heshima hiyo ili mwananchi kutoka taifa lolote aweze kuishi nchini humo kwa uhuru.
“Zanzibar kwetu ni chuo imetufunza kuishi kwa mwananchi wa taifa lolote kuwa huru bila ya kubughudhiwa na mtu elimu hiyo ambayo na sisi kwenye nchi yetu tunaiendeleza na tunapigania iendelee ili kulinda heshima ya India,” alisema.
Kuhusu ugonjwa wa corona ulioikumba dunia, Balozi Singh, alisema nchi yake ni miongoni mwa taifa lililoathirika ingawa haikupata athari katika maswala ya chakula.
Alisema kutokana na nchi hiyo kuweka mbele suala la kilimo imesaidia wakati dunia inakabiliwa na ugonjwa huo kutoathirika kwa kukosa chakula.
Januari 26 ya kila mwaka watu wenye asili ya India ambao wapo kwenye nchi mbali mbali duniani huungana na wenzao kuadhimisha uhuru ambapo mwaka huu wametimiza miaka 72.