TEHRAN,IRAN

IRAN imekanusha kuwashikilia kama mateka mabaharia wa meli iliyoikamata katika ujia wa bahari wa Hormuz, ikiituhumu kuvunja sheria za kimazingira.

Meli hiyo, MT Hankuk Chemi yenye kupeperusha bendera ya Korea Kusini, ilikuwa na mabaharia 20 wenye uraia wa mataifa mbali mbali.

Hata hivyo, Iran bado inaishinikiza Korea Kusini kuachia dola bilioni saba za Iran inazozishikilia chini ya vikwazo vya Marekani.

Msemaji wa serikali ya Iran Ali Rabiei alisema shutuma za utekaji nyara zinapaswa kwenda kwa Korea Kusini, aliyosema inazishikilia fedha za Iran bila sababu yoyote.

Inaaminika kuwa kuikamata meli hiyo ni njia ya Iran kupeleka ujumbe kwa rais mteule wa Marekani Joe Biden ambaye atachukuwa madaraka katika muda wa majuma mawili.

Iran inataka Biden aiondolee vikwazo vilivyowekwa na mtangulizi wake Donald Trump.

Korea Kusini imetuma ujumbe wa kidiplomasia mjini Tehran kujaribu kuutanzua mzozo wa meli hiyo.