NA MWAJUMA JUMA

KLABU ya soka ya Yanga imeshindwa kutamba mbele ya Jamhuri kwa kulazimishwa sare bila ya kufungana kwenye mchezo wa kombe la mapinduzi uliochezwa usiku wa kuamkia jana.

Mchezo huo ambao mashabiki wengi hawakuamini kilichotokea ulichezwa katika uwanja wa Amaan.

Katika mchezo huo ambao ni wa ufunguzi mgeni rasmi alikuwa ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman.

Miamba hiyo ambayo ilikuwa ikishambuliana kwa zamu ilikwenda mapumziko wakiwa hakuna ambae aliona mlango wa mwenziwe.

Kipindi cha pili mashambulizi yakaendelea, huku Yanga ikiliandama kila wakati lango la wapinzani wao, wakajikuta mashuti yao yote yakiishia miguuni kwa walinzi wa Jamhuri.

Jamhuri ambayo ilitoa mchezaji bora wa mchezo huo Ali Juma na kuzawadiwa pesa taslimu na Shirika la Bima la Taifa Tanzania (NIC), walionesha kiwango cha hali ya juu ambacho hakuna ambae aliweza kufikiria.

Timu hizo zilijaribu kufanya mabadiliko ya mara kwamba lakini hadi mwamuzi wa mchezo huo Nassir Msomali anapuliza kipyenga cha kumalizia dakika 90 matokeo yakabaki 0-0.

Michuano hiyo ambayo inashirikisha timu tisa itaendelea leo kwa kuchezwa mchezo mmoja utakaowakutanisha Azam na Mlandege saa 2:00 usiku.