NAIROBI,KENYA
WATU wa jamii ya Washona nchini Kenya wanasherehekea hadhi yao mpya kama raia wa nchi hiyo baada ya miongo kadhaa ya kutokuwa na nchi.
Dube ni mmoja kati ya Washona karibu 1,700 na Wanyarwanda 1,300, ambao walipata hadhi hiyo ya kisheria mwezi huu baada ya miongo kadhaa ya kutokuwa na nchi.
Desemba 12, wakati Kenya ilipoadhimisha miaka yake 57 ya uhuru, Nazizi, na wengine wa jamii ya Washona nchini Kenya walitambuliwa kama raia, kufuatia agizo la Rais Uhuru Kenyatta wa nchi hiyo.
“Changamoto zote ambazo tulipitia na hali ya kutokuwa na utaifa,tulifurahi sana kujua kwamba yote haya yameisha, ulikuwa mwanzo mpya.” Alisema Nazizi Dube.
Diana Gichengo, wa Tume ya Haki za Binadamu ya Kenya, alisema kwamba miongo kadhaa ya kutokuwa na utaifa iliiacha jamii hiyo ikitengwa.
“Walipokuwa hawana utaifa haki zao zote zilikiukwa, uhuru wao wa kutembea ulikiukwa, wasingeweza kuondoka nchini, wale wachache waliofanikiwa kusafiri walilazimika kupata vitambulisho bandia au visivyo vya kawaida kusafiri, hawakuweza kupata elimu.” Alisema Gichengo.
Washona walianza kuwasili Kenya katika miaka ya 1930, kutoka Zimbabwe, na wengi zaidi walikuja mwanzoni mwa miaka ya 1960 wakiwa wamishonari.
Wakati Kenya ilipopata uhuru wake kutoka kwa Uingereza mwaka 1963, wengi walishindwa kutumia fursa ya muda wa miaka miwili kuwa raia, pamoja na watoto wao waliozaliwa nchini humo.
Wanja Munaita wa Tume ya Umoja wa Mataifa ya Wakimbizi, alikubali uamuzi wa kuwapatia uraia washona.
“Utambulisho wa kisheria ni muhimu sana haswa kwa kuwa Kenya inaingia kwenye vitambulisho vya dijitali kwa sababu wangeachwa nje ya mfumo huo, kwa sababu hawakuwa na hati hizo.” Alisema Munaita
Gichengo wa Tume ya Haki za Binadamu ya Kenya, ambayo ilihusika katika kampeni ya kukomesha ukosefu wa utaifa, alisema mengi zaidi yanahitaji kufanywa ili kusaidia jamii ya Washona.
“Tunatumai kuwa wanaweza kuungwa mkono na serikali ya kitaifa na serikali ya kaunti kwa suala la hatua ya kuthibitisha, kuendana na miaka ambayo walitengwa.” Alisema Gichengo.
Shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa linasema Kenya ni nyumbani kwa watu wapatao 18,000 wasio na utaifa, wengi wao wakiwa makabila madogo.