NA ASYA HASSAN

JAMII imesisitizwa kuendelea kuchukua tahadhari pamoja na kufuata miongozo inayotolewa na Wizara ya afya, ili kuweza kujikinga na maradhi ya mripuko ikiwemo corona.

Wito huo umetolewa, Dk. Sanaa Said, kutoka hospitali kuu ya Mnazimmoja alipokuwa katika semina ya siku moja ya kutengeneza ujumbe juu ya kujikinga na virusi vya corona, hafla ambayo imefanyika katika ukumbi wa mtakwimu wa serikali uliyopo Mazizini.

Alisema hatua hiyo itasaidia jamii kubakia salama pamoja na kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Dk. Sanaa, alifahamisha kwamba licha ya kuwa sasa Zanzibar hakuna maradhi hayo, lakini jamii inasisitizwa kuendelea kuchukua tahadhari pamoja na kujikinga kwani baadhi ya nchi nyengine maradhi hayo yapo na wageni kutoka sehemu tofauti wanaingia ndani ya visiwa hivi.

Hata hivyo, Dk. huyo aliendelea kutumia fursa hiyo kuisisitiza Taasisi ya Panje Project kuendelea kuiunga mkono serikali katika kutoa elimu hiyo, kwani itachochea jamii kujikinga pamoja na kufika haraka vituo vya afya pale wanapoona wanadalili ya maradhi hayo.

“Afya ni kitu muhimu kwa binadamu kwani ndio chachu ya kuwawezesha kufanya shughuli mbali mbali za maendeleo na kuchochea ukuwaji wa uchumi,”alisema.

Meneja wa Taasisi hiyo, Muhammad Suleiman Said, alisema wameamua kutoa mafunzo hayo, ili kuiunga mkono serikali juu ya kupambana na ugonjwa huo.

Akizungumzia mkutano huo, alisema wameamua kufanya mkutano huo ili kupata ujumbe ambao wataupeleka kwa jamii kwa lengo la kuchukua tahadhari juu ya kujikinga na maradhi hayo.

Alifahamisha kwamba elimu hiyo itatolewa kwa njia ya vitendo ambayo watapita katika vyuo vya madrasa, skuli na kuweka mikutano kwa wanajamii ili kuwakumbusha kuendelea kuwa na tahadhari.

Meneja huyo alisema katika kufanikisha suala hilo watahakikisha wanashirikiana na wadau mbalimbali wa serikali na binafsi ili kuona lengo linafanikiwa kwa asilimia kubwa.

Baadhi ya washiriki wa semina hiyo walisema ni muhimu kwa kila binadamu, hivyo ni vyema kufuata maelekezo ya wataalamu ili kuweka usalama wao binafsi na jamii inayowazunguka.

Hata hivyo, washiriki hao walitumia fursa hiyo kuwasisitiza wananchi pale wanapoona dalili ya kuugua maradhi ya aina yoyote kufika vituo vya afya haraka ili kujiokoa wenyewe lakini pia kuzua maradhi hayo yasiwapate watu wengine.

“Endapo jamii ikiwa haipotayari kufuata maelekezo na kuchukua tahadhari kutasababisha kutokezea athari mbalimbali ikiwemo kupoteza nguvu kazi ya taifa pamoja na kuporomoka kwa uchumi,”walisema.

Mkutano huo wa siku moja umeandaliwa na taasisi ya panje kupitia mradi wa ushiriki wa afya ya jamii juu ya kupunguza athari za maradhi ya mripuko ikiwemo maradhi ya corona (CHARR) ambao utafanya kazi katika mikoa yote ya Unguja na Pemba.