NA ASYA HASSAN
KAMPUNI za bima zimeitaka jamii kuwa tayari kukata bima mbalimbali ili ziwasaidie kujikinga na majanga yanayowakuta katika mzunguko wa maisha yao.
Maofisa kutoka kampuni hizo walisema hayo walipokuwa wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, walisema hivi sasa kuna makampuni mengi yanayotoa huduma za bima hivyo ni vyema kuzitumia kampuni hizo ili ziweze kuwasaidia katika maisha yao.
Walifahamisha kwamba kampuni za bima zimekuwa na mchango mkubwa katika kuokoa maisha ya mtu mmoja mmoja, familia, taasisi na hata kampuni pale inapopata majanga ya mafuriko, kuunguliwa na hata kupoteza mali hivyo ni vyema jamii kuzitumia kampuni hizo ili kuhakikisha usalama wa mali zao.
Ofisa wa kampuni ya Bumaco Insurance, Mohammed Othman Khatib, alisema wao katika kampuni yao wanatoa huduma mbalimbali za bima ikiwemo bima ya vyombo vya moto, bima za makampuni, nyumba za watu binafsi, bima za wafanyakazi na nyenginezo.
Alisema ni vyema jamii kuchangamkia fursa hizo kwa kwenda kukata bima ya mali zao ili kupata faida ya vitu vyao pale vinapopatwa na majanga mbalimbali.
Alifahamisha kwamba umefika wakati kwa jamii kuchangamkia mpango huo ili kujikinga na changamoto za mara kwa mara zinazotokea katika mfumo mzima wa maisha yao na kusababisha kupoteza mali zao au kuwa na ulemavu.
“Wananchi wakijiunga na kampuni za bima zinawasaidia kujihakikishia usalama wa mali zao kutokana na kiasi walichowekeza kufidiwa,” alisema.
Ofisa wa kampuni ya bima ya Mayfair Insurance, Livinus Mberwa, alisema mwamko wa jamii juu ya kununua huduma za bima bado ni changamoto hivyo elimu zaidi inahitajika ili waweze kujua umuhimu wa kukata bima na kuweza kuwasaidia katika maisha yao wanapokutwa na majanga.
Alifahamisha kwamba kampuni yao imekuwa ikitoa elimu kwa jamii kupitia njia mbalimbali ikiwemo mitandao ya kijamii pamoja na vyombo vya habari ili kuona wananchi wanapata uelewa juu ya umuhimu wa kukata bima na kuweka usalama wa mali zao.
Kampuni hiyo hutoa huduma ya bima mbalimbali ikiwemo magari, nyumba, vyombo vya baharini, mizigo na nyenginezo.