NA MWAJUMA JUMA

UONGOZI wa timu ya soka ya Jang’ombe boys umemsimamisha mchezaji wake Ali Jecha Haji ‘Alcatara’ kwa muda usiojulikana kutokana na utovu wa nidhamu.

Mchezaji huyo alianza kutumikia adhabu yake hiyo kuanzia Januari 26 mwaka huu, kwa kudaiwa kuwa amekuwa na utovu wa nidhamu ambao hujirejea mara kwa mara.

Kwa mujibu wa barua ya timu hiyo iliyosainiwa na Katibu wake Alawi Haidar Foum ilieleza kuwa uongozi huo umechukuwa uwamuzi huo baada ya kuonywa mara kwa mara.

Barua hiyo iliendelea kusisitiza kwamba klabu yao imekuwa ikitoa mafunzo ya mara kwa mara kila mwisho wa mwezi kwa wachezaji wake ambayo husisitiza suala zima la nidhamu na kufuata taratibu za timu.

Sambamba na hayo uongozi wa timu unawakumbusha wachezaji wote kufUata misingi ya kiuchezaji iliyowekwa kwenye timu na kufahamu kwamba ana haki sawa na mwenziwe.

“Hii ni timu na kila mchezaji ajuwe kwamba ana haki na sawa na mwenziwe hakuna ambae yupo juu kwa mchezaji mwengine kwenye timu hii, ilisisitiza sehemu ya barua hiyo.

Boys ambayo mastakimu yake yapo Jang’ombe inashiriki ligi daraja la kwanza kanda ya Unguja, ipo nafasi ya saba ya msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi saba.