NA MWAJUMA JUMA

TIMU za Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wanaume na wanawake zimetwaa ubingwa wa michuano ya kombe la mapinduzi kwa mpira wa Wavu baada ya kufikisha pointi 15.

Michuano hiyo ambayo ilikuwa ikichezwa kwa mtindo wa ligi ilikuwa ikichezwa katika kiwanja cha Mafunzo.

JKT wanaume ilitwaa nafasi hiyo baada kushinda michezo yake yote mitano iliyocheza.

Nafasi ya pili ya michuano hiyo ilichukuliwa na Polisi ambao walijikusanyia pointi 11 wakati mshindi wa tatu ni Mafunzo ambao wana pointi nane.

Bingwa katika michuano hiyo alipata zawadi ya kikombe ambacho alikabidhiwa na mwakilishi wa Jimbo la Amaan Rukia Mapuri.

Mbali na zawadi hiyo ya kikombe kwa bingwa pia kulitolewa vyetu vya ushiriki kwa timu zote ambazo zilishiriki michuano hiyo.

Jumla ya timu sita zilishiriki katika michuano hiyo kwa upande wa wanaume zikiwemo tano za Zanzibar na moja ya Tanzania Bara.

Timu hizo ni JKT, Polisi, Mafunzo, Nyuki, MTS na Makoba.Kwa upande wa wanawake JKT ilitwaa ubingwa baada ya  ushindi wa seti 3-0 dhidi ya Mkalapa.

Timu tatu za wanawake zilishiriki michuano hiyo ambayo iliandaliwa na Chama cha Mchezo huo Zanzibar (ZAVA), ambayo ni mara ya kwanza kushirikisha timu kutoka Tanzania Bara.