BEIJING,CHINA

POLISI katika eneo la Hong Kong wamesema wamewakamata watu wawili zaidi kwa tuhuma za kukiuka sheria ya usalama wa taifa ya eneo hilo.

Polisi walitangaza kukamatwa kwa wawili hao ambapo vyanzo vya habari vinasema wawili hao ni wanaharakati wa demokrasia Joshua Wong na Tam Tak-chi.

Wote walikuwa tayari gerezani wakati wa kukamatwa kwao wanashtakiwa kwa uasi.

Wong alikuwa gerezani tangu alipohukumiwa mwaka jana kwa kuchochea na kushiriki maandamano nje ya makao makuu ya polisi mwaka 2019.

Tam amekuwa gerezani baada ya kutuhumiwa kwa mashitaka tofauti.

Polisi walisema ukamataji huo unahusiana na uchaguzi usiokuwa rasmi ulioandaliwa na wanaharakati wa demokrasia ili kuchagua wagombea wa uchaguzi wa Baraza la Bunge uliopangwa kufanyika mwezi Septemba lakini ukaahirishwa.

Mwanachama wa zamani wa Baraza la Bunge Raymond Chan Chi-chuen aliachiliwa huru baada ya kuzuiliwa kwa karibu masaa 40.

Chan alisema kukamatwa kwake ni upuuzi mtupu kwa sababu kile yeye na wengine walichodhamiria kushinda kupitia uchaguzi huo ni haki zinazolindwa na Sheria mama, ambayo inatumiwa kikamilifu kama katiba ya Hong Kong.