NA HAFSA GOLO

JUMUIYA ya Wazazi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) jimbo la Mfenesini imetakiwa kuandaa mbinu zitakazosaidia mapambano dhidi ya vitendo vya udhalilishaji sambamba na kuwafichua wale wote  watakaobainika kujihusisha  na vitendo hivyo ili sheria ichukue nafasi yake.

Mwakilishi wa Jimbo la Mfenesini, Machano Othman Said alitoa wito huo alipokua akifungua mkutano wa jumuiya hiyo uliofanyika Kama.

Machano aliwataka wanajumuiya hiyo kuondokana na muhali, urasimu juu ya vita hivyo ambavyo vimekuwa vikidumaza haki na stahi za wanawake na watoto nchini pamoja na juhudi zinazochukuliwa na serikali.

Alisema ipo haja kwa wanachama hao  kushirikiana  na kubuni njia bora za uhamasishaji  kwa jamii iliyowazunguka  pamoja na  kuungana na serikali za mitaa katika vita vya udhalilishaji ikiwemo kuelimisha umuhimu wa utoaji wa ushahidi katika vyombo vya sheria.

Aidha, alisema hatua hiyo iwe pamoja na kukabiliana na vitendo vya utumiaji wa dawa za kulevya na wizi wa mazao.

Machano alisema suala la ulinzi wa mazingira katika maeneo yao ili kudhibiti wimbi la ukataji wa miti ovyo sambamba na uchimbaji wa mchanga holela.

 Katika hatua nyengine mwakilishi huyo ,aliwasihi kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya nane kwenye kupiga vita ufisadi,rushwa na matumizi mabaya ya rasilimali za umma.

Kwa upande wa wanajumuiya hiyo, waliahidi kuyatekeleza maelekezo hayo ikiwa ni sambamba na kuandaa mikakati na mipango ya kuleta maendeleo jimboni humo.