NA HAJI NASSOR

KAMATI ya kupambana na udhalilishaji na ukatili wa wanawake na watoto ya wilaya ya Chake Chake, imempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, kwa malengo yake ya kupungumza wimbi la udhalilishaji nchini.

Hayo yalielezwa na mjumbe wa kamati hiyo, Kassim Ali Omar alipokuwa akizungumza katika kikao kilichofanyika Chake Chake.

Alisema tamko la Dk. Mwinyi alilolitoa hivi karibuni wakati akizungumza na wadau wa vitendo hivyo, linathihirisha azma yake ya kukabiliana na udhalilishaji.

Alisema kwa muda mrefu wanaumizwa na sheria zinazoshughulikia vitendo hivyo jinsi zilivyo nyepesi na kusababisha vitendo hivyo kuongezeka.

Mjumbe wa kamati hiyo, Zuwena Hamad Ali, alisema changamoto za baadhi ya watendaji zitatatuliwa ili vitendo hivyo vikome.

Alisema wakati mwengine uhaba wa vietendea kazi na rasilimali watu, huchangia kwa kiasi kikubwa kuendelea kutokea kwa vitendo hivyo.

Akifungua mkutano huo, Katibu tawala wilaya ya Chake Chake, Omar Juma alizitaka taasisi zinazopambana na udhalilishaji kwenda ofisini kwake kama watakuwa na  changamoto.

Aliipongeza kamati hiyo, kwa juhudi inazochukua kuifikia jamii kuwapa elimu ya mbinu za kuripoti matukio hayo.

“Kamati hii imefanyakazi kubwa na ndio sababu mwaka 2019 kulikuwa na matukio 200, lakini mwaka jana kulikuwa na matukio 105, jambo linalotia moyo,” alisema.

Aliwahimiza wajumbe kuendelea kufanya kazi kwa bidii na ushirikiano kwani nguvu za pamoja ndio silaha pekee.

Mapema akiwasilisha muongozo wa malezi ya mtoto kwa mlezi, Ofisa idara ya ustawi wa jamii, hifadhi ya mtoto wilaya ya Chake Chake, Rashid Said Nassor, alisema mradi huo upo kwenye shehia tano kwa njia ya majaribio.

Alisema shehia hizo ni Ziwani, Wawi, Kichungwani, Matale na Madungu, ambazo zilionekana kuwa na tatizo kubwa la udhalilishaji.

Kamati hiyo ni zao la mkutano wa rais mstaafu wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, uliofanyika 2017.