NA OTHMAN KHAMIS, OMPR

KAMPUNI ya semcrete kutoka nchini Misri inayojihusisha na ujenzi wa miundombinu ikiwemo bandari, barabara, afya, maji, elimu na umeme, imeonesha utayari wa kutaka kuwekeza miradi yake visiwani Zanzibar.

Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Sherif Nazmy alitoa kauli hiyo wakati ujumbe aliouongoza ulipofanya mazungumzo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla huko ofisini kwake Vuga mjini hapa.

Sherif alisema kutokana na mazingira rafiki ya uwekezaji yaliyopo Zanzibar uongozi wa kampuni yake muda wowote kuanzia sasa utawekeza mradi wake wa kwanza ambao utapitishwa na kuthibitishwa na serikali ya Mapinduzi.

“Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ina fursa ya kuchagua miundombinu yoyote ambayo kampuni yetu itakuwa tayari kuanza nayo katika muelekeo wa kuzitumia fursa za uwekezaji”, alisema Sherif.

Mkurugenzi huyo alimueleza Makamu wa Pili wa Rais, kwamba hatua hiyo ya uongozi wa taasisi yake kutaka kuwekeza Zanzibar inalenga kuona ustawi wa wananchi wa Zanzibar unaendelea kuimarika.

Mapema ofisa mkuu wa kampuni hiyo Sherif Sabry alisema kampuni yao iko makini wakati wote katika kuzingatia taaluma pamoja na fedha ili kuhakikisha miradi inayoanzisha inakamilika kwa wakati.

Sabry alisema kampuni ya semcrete tayari imejipatia uzoefu wa kutosha kwa miaka mingi ikiendelea kusambaa katika pembe mbali mbali za dunia, Afrika ikiwemo Tanzania hasa katika uendelezaji wa miradi ya miundombinu ya barabara na maduka makubwa.

Akitoa shukrani zake, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla aliueleza uongozi huo wa kampuni hiyo kwamba serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejidhatiti katika kuhakikisha miradi ya uwekezaji inafanikiwa vyema.

Hemed  alilazimika ndani ya mazungumzo na uongozi huo kuwasiliana moja kwa moja kwa njia ya simu na waziri anayesimamia masuala ya uchumi na uwekezaji Zanzibar, Mudrik Ramadhan Soraga na kumuagiza kukutana na uongozi wa kampuni hiyo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza uongozi wa kampuni ya semcrete kwa nia yake ya kutaka kuzitumia fursa za uwekezaji zilizopo Zanzibar na kuahidi kwamba serikali itashirikiana nao vyema ili yale malengo yaweze kutimia.