NA TATU MAKAME
USHIRIKA wa waumini wa dini ya kikristo kanisa la Tanzania Assemblies of God la Jumbi mkoa wa Kusini Unguja, wamefanya kazi ya kuweka mji katika hali ya usafi eneo la kanisa hilo pamoja na skuli ya msingi ya Jumbi.
Akizungumza mara baada ya kukamilika kwa zoezi hilo Mchungaji wa kanisa hilo, Joakim Salia Asunevila, alisema wamefikia hatua hiyo mara baada ya kupata agizo la Rais pamoja na kutafakari kwa kina juu ya umuhimu wa usafi katika jamii hivyo wameamua kuelekeza usafi huo katika maeneo ya kijamii.
Aidha aliahidi kutoa ushirikiano mkubwa kwa serikali ya awamu ya nane chini ya Dk. Hussein Ali Mwinyi katika nyanja mbalimbali ikiwemo suala zima la kuweka mazingira katika hali ya usafi.
Aliwaomba viongozi wa makanisa na misikiti kwa kushirikiana na waumini wa dini nyengine kuiunga mkono serikali katika kuhakikisha wanaweka mazingira katika hali ya usafi ili kuvutia watalii.
Azungumza kwa niaba ya waumini wenzake, Herieth Martin Shenyangwa, alisema suala la usafi ni la kila mwananchi hivyo aliwaomba kuwa na utaratibu wa kusafisha maeneo yao mara kwa mara, kwani kufanya hivyo kutawafanya waishi maeneo safi pamoja na kuondokana na maradhi mbalimbali yanayosababishwa na uchafu wa mazingira.
Kwa upande wake Sheha wa Shehia ya Jumbi, Muhidini Haji Machano, aliushukuru uongozi wa kanisa hilo kwa kutekeleza agizo hilo la usafi, huku akiwataka wananchi wenye maboma katika shehia hiyo kuyasafisha mara moja na atakaekaidi agizo hilo atachukuliwa hatua za kisheria.