NA MWAJUMA JUMA

KOCHA mkuu wa timu ya soka ya Yanga Cedric Kaze amesema wachezaji alionao katika kikosi kinachoshiriki mashindano ya kombe la mapinduzi kina uwezo mkubwa wa kutwaa taji hilo.

Kocha huyo alitoa kauli hiyo mara baada ya mchezo dhidi ya Jamhuri ambao ulimalizika kwa sare ya bila kufungana, hali iliyoonekana kwamba matokeo hayo yametokea kutokana na kuwakosa baadhi ya wachezaji wake.

Alisema mabadiliko katika kikosi chake ni maamuzi ya ufundi kutokana baada ya wachezaji wengi kutumika sana katika mechi za ligi na walihitaji muda wa kupumzika.

“Wachezaji wametumika sana kwenye ligi tunatoka kwenye ziara ya mikoani na siku 21, tulicheza mechi nne sasa kuna wachezaji wengine wamechoka sana wanahitaji wapumzike”, alisema.

Hivyo alisema anaamini kwamba wachezaji waliopo katika kikosi chake wana uwezo wa kutosha wa kucheza katika mashindano hayo na ndio maana wakapewa nafasi za kucheza.

Alifahamisha kwamba katika mechi hiyo wamecheza vizuri na wachezaji ambao wametokea U-20 wamecheza vizuri na kuonesha uwezo wao.

Aidha alisema watajipanga katika mechi yao ya kesho na Namungo saa 2:15 usiku ili kuweza kufanya vizuri zaidi na kuondoka na matokeo ambayo yataiweka timu yake katika mazingira mazuri.

Alisema wachezaji 11 kutoka kila upande walishindana na kilichotokea ni moja ya matokeo ya mchezo.

Yanga ipo katika kundi A likiwa na timu za Jamhuri na Namungo.