NAIROBI, KENYA
TUME ya uchaguzi ya nchini Kenya imeidhinisha mswada wa marekebisho ya katiba ya nchi hiyo wenye lengo la kuwaunganisha wananchi wa Kenya.
Mswada huo umekuja maelewano baina ya rais wa nchi hiyo chini hiyo Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga na kuanzisha mridhiano yanayojulikana kama BBI.
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Wafula Chebukati aliwaandikia marais wa mabunge yote 47 ya kaunti na kuuwasilisha rasmi mswada huo.
Viongozi wa kidini wamegawanyika kuhusu suala la mageuzi ya katiba na kura ya maoni inayonukia nchini Kenya. Kinyume na ilivyokuwa mwaka 2010, viongozi wa makanisa wana mitazamo tofauti.
Kanisa katoliki nchini Kenya limeashiria kuwa huenda likaipinga kura ya maoni kwani inaweza kuleta migawanyiko, kuwa na gharama nyingi kadhalika ubadhirifu.
Kwa upande mwingine kanisa la kianglikana la Kenya lililo na sauti kubwa kuhusu mageuzi linakiri kuwa muda umewadia kuifanyia katiba ya Kenya mabadiliko.
Hivi karibuni baraza kuu la makanisa lilitoa ishara kuwa huenda likaunga mkono kura ya maoni ila mchakato huo lazima ujikite kwenye kuwapa kipaumbele Wakenya wenyewe na mahitaji yao.
Wakati huo huo makanisa ya protestanti yanashauri kura ya maoni kufanyika iwapo itawaunganisha pamoja Wakenya.
Mwishoni mwa mwezi Agosti 2020, rais Uhuru Kenyatta kwenye hotuba yake kwa taifa aliusisitizia umuhimu wa kuandaa hati ambayo itawanufaisha wakenya kwani muda umewadia kuitathmini upya katiba.