NA JOSEPH NGILISHO, ARUSHA

KESI inayowakabili askari watatu na raia watano, akiwemo Mfanyabiashara maarufu wa madini ya Tanzanite Jijini Arusha ,Lucas Mdeme{46} imechukua sura mpya baada ya Askari wa Magereza kuzuia waandishi kufanya kazi zao.

Askari na raia hao wanakabiliwa na mashtaka sita ikiwemo uhujumu uchumi ,utakatishaji fedha haramu na kupanga njama za kujipatia fedha ya awali shilingi milioni 10 kati ya milioni 30 walizohitaji kutoka kwa mfanyabiashara was Madini ya Tanzanite, Sammy Mollel.

Kesi hiyo ilitajwa katika mahakama ya Hakimu wilaya ya Arusha, na kuhairishwa hadi Febuari 10, mwaka huu, kwa madai ya upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.  

Waendesha Mashtaka wa serikali, Adelaide Kassalay na Agnes Hyera, walimweleza Hakimu Ngoka, kuwa wanaomba tarahe nyingine ya kutajwa kwa kesi hiyo kwani upelelezi haujakamilika.

Hakimu aliihairisha kesi hiyo hadi tarehe hiyo na watuhumiwa kuendelea kukaa rumande gerezani kwa kuwa haina dhamana na mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo.

 Kabla ya kupandishwa kizimbani utaratibu mahakamani hapo ulibadilika na raia wote wenye kesi na wasiokuwa na kesi waliamuriwa na Askari Magereza kukaa nje ya geti la mahakama na waandishi kunyimwa kupiga picha na kuzuiwa kuingia ndani ya geti hilo.

Kasheshe hiyo ilimkumba mwandishi wa kike wa gazeti la Mwananchi, Husna Issa, kwani alipopiga picha alikamatwa na askari Magereza wa kiume na kufuta picha zote walizopigwa watuhumiwa hao na kukalishwa chini ya ulinzi na baadae  kutolewa nje ya geti.

Pia Mwandishi huyo, alipata kibano kutoka kwa ndugu wa watuhumiwa hao na kuambiwa kuwa asirudie tena, kwani wenyewe wameshaweka mazingira ya ndugu zao kutopigwa picha tena.

” Mmezidi kiherehere mnapiga picha tu waume zetu umeona  Cha Moto sasa!! Angalia watu wameshaweka mambo yao sawa nyie mnataka kuharibu haya sasa ” alisikika ndugu akitamba mahakamani hapo.

 Alizungumzia tukio hilo kwa njia ya simu ya kiganjani juu Askari wake kuwa na mkakati maalumu Mkuu huyo wa Magereza Mkoa wa Arusha, Widson Mwanangwa alisema hana taarifa zozote ila atafuatilia kujua ukweli, ili hatua nyengine zichukuliwe kwani kila mmoja anapaswa kufanya kazi kwa kufuata taratibu na sheria zilizowekwa.

Kabla ya kupandishwa kizimbani Askari watatu walishtakiwa kijeshi na walibainika na tuhuma na fukuzwa kazi kwa rushwa na waliopandishwa kizimbani ni pamoja na pamoja na  Askari mwenye namba G. 5134 DC Heavenlight Mushi  aliyekuwa Askari kitengo Cha Intelijensia Mkoa wa Kipolisi Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Wengine ni askari H.125 PC Gasper Paul kitengo Cha Intelijensia Makao Makuu Dodoma na H.1021 PC Bryton Murumbe aliyekuwa Askari wa kawaida Mkoani Dodoma.

Raia wengine walioshtakiwa  mahakamani mbali ya Mdeme kuwa ni pamoja na Joseph Chacha{43} maarufu kwa jina la ‘’baba Ngodo’’ mkazi wa Ilboru, Leonila Joseph{46} mkazi wa Ilboru, Mfanyabishara maarufu Jijini Arusha ,Nelson Lyimo{58} mkazi wa Kijenge Juu na Omary Alphonce{43} maarufu kwa jina la Matelephone mkazi wa Olasiva Jijini Arusha.