NA TATU MAKAME

SAIDI Abdalla (22) mkaazi wa Fuoni Kibondeni Wilaya ya Magharibi ‘B’ Unguja, amepelekwa rumande kusubiria kesi inayomkabili baada ya kutenda kosa la kumtorosha mtoto wa kiume aliye chini ya uangalizi wa wazazi wake.

Kesi hiyo ilisikilizwa na Hakimu Valentine Andrew Katema wa mahakama ya mkoa Vuga, baada ya Mwendesha Mashitaka, kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Ahmed Mohamed, kumsomea kosa mshitakiwa huyo.

Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, mshitakiwa huyo mnamo Februari 5 mwaka 2019 majira ya saa 10:00 alaasiri, mshitakiwa huyo alitenda kosa la kumtorosha mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka saba (jina linahifadhiwa), kinyume na kifungu cha 113 (1) (b) cha sheria namba 6 ya mwaka 2018 sheria za Zanzibar.

Kosa la pili ni kumlawiti mtoto aliye chini ya uangalizi wa wazazi wake, kinyume na kifungu cha 115 (2) cha sheria namba 6 ya mwaka 2018, jambo amablo ni kosa kisheria.

Ilidaiwa kuwa, siku hiyo mnamo Februari 5 majira ya saa 10:00 mshitakiwa huyo alimlawiti mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka saba, kitendo ambacho ni kosa kisheria.

Hata hivyo mshitakiwa huyo yupo rumande kutokana na kuwa kesi yake haina dhamana na kuahirishwa kwa ajili ya kusikilizwa Januari 11 mwaka huu.