NA HUSNA SHEHA

MAHAKAMA ya Mkoa Mahonda, imepeleka rumande Ramadhan Hamad Suleiman (18) mkaazi wa Mahonda  Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Mkoa wa Kaskazini Unguja, akikabiliwa na tuhuma za kubaka mtoto wa miaka 15.

Hakimu wa mahakama hiyo Makame Khamis Ali,  alimuamuru kijana huyo kwenda rumande, kutokana na shitaka aliloshitakiwa nalo ni miongoni mwa mashitaka yasiyokuwa na dhamana.

Mapema mshitakiwa huyo alisomewa makosa yake na Mwendesha Mashitaka, Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Khamis Othman.

Katika mashitaka hayo, mshitakiwa huyo alidaiwa kumuingilia kimwili msichana mwenye umri wa miaka 15 (jina linahifadhiwa), kitendo ambacho ni kosa kisheria.

Upande huo wa mashitaka ulidai kuwa, mshitakiwa huyo alidaiwa kumfanyia kitendo hicho msichana huyo, mnamo mwezi wa Disemba mwaka 2018 majira ya saa 3:30 za asubuhi, huko Mahonda Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka iliyowasilishwa mahakamani hapo inadai kuwa, kitendo cha kubaka  msichana ni kinyume na vifungu vya 108 (1) (2) (e) na 109 (1) vya sheria namba 6 ya mwaka 2018  sheria za Zanzibar.

Kabla ya hapo, siku hiyo mshitakiwa huyo bila ya halali alidaiwa kumtorosha mtoto huyo aliye chini ya uangalizi wa wazazi wake majira ya saa 3:00 za asubuhi, kwa kumtoa nyumbani kwao Mahonda bila ya ridhaa ya wazazi wake.

Alidaiwa kutenda kitendo hicho kinyume na kifungu cha 113 (1) (a) cha sheria namba 6 ya mwaka 2018 sheria za Zanzibar.

Baada ya kusomewa mashitaka yake mshitakiwa huyo alikataa na upande wa mashitaka kudai kuwa, upo tayari kuthibitisha tuhuma hizo walizoziwasilisha.