NA KIJA ELIAS, HAI

DIWANI wa Kata ya Masama Kusini Cedrick Pangani, amewasisitiza Wanawake, Vijana na Watu wenye ulemavu kuendelea kujiunga kwenye vikundi, ili waweze kufikiwa kwa urahisi kwenye mikopo  inayotolewa na hamlashauri  ili fedha hizo ziweze kuwasaidia kuwainua kiuchumi.

Hayo aliyasema jana wakati  wa ziara yake ya kuvitembelea vikundi vilivyopo ndani ya kata yake ambavyo vinanufaika na asilimia 10 ya mapato ya ndani yanayotolewa na halmashauri ya Wilaya ya Hai.

Akizungumza na Kikundi cha Wajane, Wagane na Wapweke (WANA WA ASAFU), kilichopo chini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Ushirika wa Makuna Mtaa wa Majengo wilayani humo, Diwani Pangani aliwataka Wanawake Vijana na Watu wenye ulemavu ili waweze kunufaika na mikopo hiyo.

Alisema vipo vikundi vingi vimekuwa vikipata mikopo, lakini havina elimu ya kutosha ya namna ambavyo vinaweza kuitumia kikopo hiyo kwa ajili ya kuendesha miradi ya kiuchumi.

“Naomba nitoe wito kwa wanufaika wa mikopo hii kuhakikisha kwamba fedha wanazopewa zinakwenda kutekeleza miradi  au biashara walizokusidia na kujenga tabia ya kuzirejesha kwa wakati ili  ziweze kunufaisha vikundi vingi zaidi kama inavyotarajiwa,”alisema.

Alisema  ziara hiyo imelenga kukutana na vikundi ambavyo vinanufaika na asilimia 10 ya mapato ya ndani yanayokusanywa na halmashauri ya Hai, hivyo nimeamua kuvitembelea vikundi hivi kwani kuna vingine havijui namna ya kuomba mikopo hiyo na vikundi vingine vimekuwa vinapata mikopo hiyo lakini havina elimu yakutosha.

“Katika ziara yangu hii nimelazimika kuambatana na Wataalam wa Maendeleo ya Jamii wa Kata, ili kuvipitia vikundi  vyote vilivyonufaika na mikopo hii ili kuwaelimisha na kuwasikiliza changamoto wanazokumbana nazo,”amesema.

Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii Kata ya Masama Kusini, Lilian Loth, alisema  vikundi vingi vilivyopo katika kata hiyo havipendi kusajiliwa kwa kuhofia kupoteza muda wao wa kuzalisha mali na kukaa kwa ajili ya kutengeneza Katiba.

“Katika kata yangu vipo vikundi vingi havijasajiliwa, vikundi vilivyosajiliwa hadi sasa ni vikundi 18 tu, lakini kuna vikundi vingine vinapoomba mkopo na kiushindwa kupata vimekuwa vikikata tamaa ya kuomba mkopo hali ambayo inapelekea kujiondoa kwenye vikundi vya ujasiriamali,’amesema Loth.

Mwenyekiti wa Kikundi cha Wajane, Wagane na Wapweke Jane Massawe, alisema  vikundi vingi havijapata elimu ya kuomba mikopo  kutoka halmashauri na kuiomba serikali kupitia kwa maafisa Maendeleo ya Jamii kuvitembelea vikundi vilivyopo vijijini ili viweze kupata elimu hiyo ya mikopo.

Katibu wa kikundi hicho Elisamia Munisi, alisema ni vema kabla vikundi hivyo havijapewa mikopo ni vyema vikapatiwa elimu vikundi vingi vimekuwa vikikimbilia kuomba mikopo lakini hawana mradi ambao wanakwenda kuufanya jambo ambalo limekuwa likipelekea kushindwa kuirudisha mikopo hiyo.

Kwa upande wake mtendaji kata ya Masama Kusini Emanuel Simoni, alitoa wito kwa vikundi ambavyo vimefanikiwa kupata mikopo kwenye halmashauri hiyo kurejesha mikopo yao kwanza ndipo wakope tena.

“Wapo baadhi ya vijana wengi wamekuwa wakikosa sifa ya kupata mikopo kutokana na kutopenda kujiunga  katika vikundi  kutokana na wengi kutokuwa na makazi maalumu ya kuishi,”alisema.