NA MWAJUMA JUMA

TIMU ya soka ya Kilimani City juzi ilimpokea kocha wake mpya kutoka Giovani Scanu na msaidizi wake Nicola Calvia, ambao wataifundisha timu hiyo inayoshiriki ligi daraja la kwanza Kanda ya Unguja.

Kocha huyo ambae ataifundisha timu hiyo kwa mkataba wa miezi mitatu  aliwasili juzi visiwani Zanzibar na kupokewa na uongozi wa timu hiyo.

Akizungumza ujio wa kocha huyo Afisa Habari wa timu hiyo Zainab Haroub  alisema kocha ataifundisha timu kwa mashirikiano ya karibu na makocha waliokuwepo sasa.

Alisema kwa kuwa kocha huyo amekuja na msaidizi wake na bado ni wageni watatiliana mkataba wa miezi mitatu na mambo yakiwa mazuri watawaongezea muda.

“Kwa sasa tunamuangalia kwa muda wa miezi mitatu na atakuwa anashirikiana na makocha waliokuwepo”, alisema.

Hata hivyo akizungumza mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid Amani Karume, kocha huyo alisema ujio wake ni kuhakikisha anashirikiana na viongozi wa timu hiyo ili kuifikisha ligi kuu.

“Nitatumia ujuzi wangu pamoja na jitihada zangu zote kwa kushirikiana  na wenzagu ili kuipandisha timu hiyo”, alisema.

Alisema  wanahitaji kupata mpangilio maalumu hatua baada ya hatua ili kubadilisha akili za wachezaji hao.

Alisema mpira ni kama maisha ambao bila ya kuwa na programu maalumu na kwa hatua hautafanikiwa.

Kwa upande wake rais wa timu hiyo Khamis Shaali Choum, aliwataka wadau wa timu hiyo, kumuunga mkono kocha huyo ambae atashirikiana na makocha wazawa katika kuinua timu hiyo.

Alisema kocha  huyo ana uzoefu mkubwa wa kufundisha  soka na kuwataka vijana kuwa tayari kubadilika ili waendane na mabdaiiko ya soka la kisasa.

 Hivyo aliwataka wachezaji kuchangamkia fursa hiyo ambayo itatoa mwanga mkubwa kwa maslahi yao hapo baadae.