NA PRISCA LIBAGA, ARUSHA

MKUU wa Mkoa wa Arusha Idd Hassan Kimanta ameongoza kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa (RCC) kwa mara ya kwanza akiwa mkuu wa mkoa kufuatia kuteuliwa kwake na Rais Dk. John Pombe Magufuli Juni 6, mwaka jana.

Akifungua kikao hicho mkuu huyo aliwaambia wajumbe kwamba masuala ya maendeleo hayana itikadi hivyo ni wajibu wao kusimamia kikamilifu utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi ambayo ndiyo yenye serikali iliyoko madarakani.

Kimanta aliwataka viongozi wa sekta zote pamoja na wananchi kuungana na kuwa kitu kimoja kuhakikisha wanashirikiana na kuondoa tofauti zao zilizokuwepo wakati wa kampeni na uchaguzi uliopita.

Aidha Kimanta alisisitiza suala la wananchi kulipa kodi mbalimbali za serikali kwani bila kodi kamwe serikali haiwezi kutekeleza shughuli za maendeleo wala kutoa huduma za Kijamii kwa wananchi.

Hata hivyo, aliitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA) kushirikiana na kamanda wa TAKUKURU katika mkoa huo kuhakikisha inawasaka kwa njia zote wafanyabiashara wanaokwepa kulipa kodi za Serikali.

Akitoa taarifa ya ukusanyaji wa mapato katika Kikao hicho cha RCC meneja wa TRA mkoa wa Arusha John Mwigura aliwaambia wajumbe hao wa RCC kwamba mkoa wa Arusha ni wa pili katika ukusanyaji wa mapato ya serikali baada ya mkoa wa Dar es salaam.

Mwigura alisema katika mwaka wa fedha 2020/2021 kati ya kipindi cha Julai hadi Disemba TRA wamefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 162.88 kati ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 237.90 sawa na asilimia 68 ya lengo

Hata hivyo Mwigura alisema matokeo ya makusanyo haya yanaonyesha kushuka kutoka lengo la kukusanya Shilingi bilioni 238.85 kwa kipindi cha Julai 2019/2020 hadi shilingi bilioni 162.88

Aliwaeleza wajumbe hao wa RCC kwamba TRA ililenga kukusanya kodi za ndani bilioni 204.31 hata hivyo iliweza kukusanya shilingi bilioni 197.39 sawa na asilimia 97 katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2019/2020

Aidha katika kodi hizo za ndani kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 2020/2021 TRA ililenga kukusanya Shilingi bilioni 193.45 hata hivyo ilikusanya kiasi cha Shilingi bilioni 125.55 sawa na asilimia 65.

Kuhusu ushuru wa Forodha  katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2019/2020 TRA ililenga kukusanya Shilingi bilioni 42.98 hata hivyo ilikusanya Shilingi bilioni 41.46 sawa na asilimia 96

Mwigura aidha amesema katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2020/2021 TRA imekusanya Shilingi bilioni 37.33 sawa na asilimia 84 kati ya lengo la kukusanya mapato ya Shilingi bilioni 44.45

Meneja huyo wa Mkoa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Mkoa wa Arusha alitaja baadhi ya sababu za kutofikia  malengo ya ukusanyaji wa mapato katika kipindi cha nusu ya Kwanza kwa mwaka wa fedha 2020/2021 kuwa zimechangiwa na mlipuko wa  homa ya mapafu-COVID-19