HONDURAS ni taifa lilioko Amerika ya kati lililopakana na Guatemala upande wa magharibi na kupakana na El Salvador  upande wa kusini magharibi ambapo Nicaragua iko upande wa kusini mashariki mwa taifa hilo.

Kwa upande wa kusini, Honduras imepakana na bahari kuu ya Pasifiki na ghuba ya Fonseca ambapo eneo kubwa la mwambao wa taifa hilo limeingia katika bahari ya Caribbean.

Moja ya kioja kikuu kilichoko katika taifa hilo ambacho hujitokeza kila mwaka ni kuanguka samaki wengi kutoka mbinguni katika kijiji cha Yoro kilichopo katikati ya nchi hiyo.

Kumekuwa na nadharia nyingi na simulizi nyingi za mapokezi kuhusiana na chanzo na asili ya kioja hicho kisicho cha kawaida.

Hadi leo wanasayansi wamekuwa wakitofautiana kuhusu sababu za samaki hao wengi kuanguka ardhini katika kijiji ambacho kiko katikati ya nchi hiyo mbali na bahari, maziwa au mito.

Kumbukumbu za kihistoria zinaonesha kuwa samaki wanaoanguka kijijini hapo kutoka mbinguni wamekuwa wakianguka mara moja au mara mbili kila mwaka kwa karibu miaka 200 iliyopita.

Halihiyo isiyo ya kawaida imepewa jina la “Mvua ya Samaki” ambapo mamia ya watu mitaani huokota samaki hao pale wanapoanguka.

Inasemekana kuwa katika miaka ya 1850, watu wa kijiji hicho cha Yoro walikuwa masikini mno na waliishi katika hali duni ya maisha na njaa ilikuwa ni tatizo kubwa kijijini hapo.

Katika miaka hiyo, Padri mmoja kutoka nchini Hispania aitwae Jose Manuel ambaye alikwenda huko Marekani ya Kusini kueneza dini ya kikiristo alifika kijijini hapo.

Baada ya Padri huyo kufika kijijini hapo na kuona hali duni ya maisha ya watu wa eneo hilo ndipo aliposali kwa siku tatu kumuomba Mungu awaondoshee watu hao madhila hayo.

Simulizi hizo zinaeleza kuwa baada ya Padri huyo kusali kwa siku tatu kuomba Mungu, ndipo mawingu mazito ya mvua yalipotanda mbinguni na mvua kubwa yenye dhoruba iliponyesha ikiambatana na samaki wengi walokuwa wakianguka kutoka mbinguni.

Kwa mujibu wa simulizi hizo, hiyo ndiyo ilikuwa mara ya kwanza samaki hao wengi kuanguka ardhini kutoka mbinguni.

Hapo mwaka 1823, mvumbuzi aitwae Alexander von Humbolt kutoka nchi ambayo kwa wakati huo ikijulikana kama Prussia aliandika simulizi za kuona samaki waloanguka ardhini kutoka mbinguni alipotembelea nchi ya Ecuador ambayo pia iko huko Amerika ya Kati.

Inasemekana kuwa hapo mwaka 1698 kulitokea mripuko wa Volkano katika Mlima Carihuarianzo ambapo baada ya kumalizika mripuko huo wa Volkano, eneo la maili 45 za mraba lililozunguka mlima huo lilijaa matope na samaki wengi.

Iliaminika kuwa samaki hao walokuwa wamesambaa katika eneo kubwa la ardhi linalozunguka mlima huo walitoka katika ziwa lililoungana na mlima huo chini ya ardhi ambalo watu walikuwa hawalijui kuwa ziwa hilo lilikuwa ndani ya uwazi mkubwa ulokuwa ndani ya mlima huo.

Tokea miaka hiyo ya 1850, pale PadriJose Manuel alipoomba dua na samaki hao kuanguka ardhini, hali hiyo imekuwa ikijitokeza kila mwaka nchini humo hasa wakati wa majira ya mvua kubwa kati ya mwezi wa Mei na Juni ambazo kwa kawaida, kutokana na sababu za kijografia za eneo hilo, mara nyingi mvua hizo huandamana na dhoruba kali.

Katika miaka ya 1970, mara kadhaa wanasayansi kutoka National Geographic walifika katika kijiji hicho cha Yoro nchini Honduras kufanya utafiti ili kujua sababu za kisayansi zinazosababisha samaki hao kuanguka ardhini kutoka mbinguni.

Kutokana na utafiti wao wa kina, wanasayansi hao walithibitisha kuwa samaki hao walianguka ardhini kutoka mbinguni na walishindwa kubainisha chanzo halisi walikotoka samaki hao zaidi ya kuwa walianguka kutoka mbinguni.

Mvua kama hiyo ya samaki waloanguka ardhini kutoka mbinguni ilitokea huko nchini Australia katika mji wa Lajamanu hapo tarehe 25 Februari, 2010.

Kuanguka samaki hao ardhini kutoka mbinguni huko nchini Australia kulifungua njia kwa wanasayansi kufanya utafiti zaidi ili kujua chanzo halisi cha tukio hilo lisilo la kawaida hasa kwa vile mji huo wa Lajamanu walikoanguka samaki hao uko umbali wa kilomita 200 kutoka mwambao wa bahari.

Nadharia moja iliyotolewa na wanasayansi inayosababisha samaki hao kuanguka ardhini kutoka mbinguni ni ile inayodai kuwa kutokana na mvua nyingi na kubwa kunyesha na kusababisha mafuriko makubwa ya ghafla kwa muda mfupi, samaki kutoka mito na maziwa ya mbali husombwa na mafuriko hayo na kukokotwa na maji.

Lakini mafuriko hayo yanapomalizika ndipo samaki hao hubaki ardhini na watu hudhani kuwa wameanguka kutoka mbinguni.

Hata hivyo hoja hii ni nyepesi kimantiki kwa vile samaki hao wamekuwa wakianguka katika eneo hilo hilo kila mwaka kwa zaidi ya miaka 200 sasa. Si hayo tu, bali pia samaki hao hawaonekani ardhini katika maeneo ambayo yapo karibu na mito na maziwa bali huonekana katika kijiji hicho ambacho kwa sasa kimekuwa ni mji kutokana na kujengwa majengo mbalimbali.

Ingawa hoja hiyo ni dhaifu, lakini wanasayansi wengine wanasisitiza kuwa hoja hiyo ndiyo yenye mashiko kwa vile mara kadhaa kutokana na sababu za kijografia inaponyesha mvua kubwa yenye dhoruba katika baadhi ya maeneo, mvua hiyo husababisha mafuriko ambayo huwafanya baadhi ya viumbe wanaoishi majini kama vile vyura, mamba, samaki, nyoka na hata baadhi ya ndege kusombwa na maji hayo na kutupwa katika maeneo ya mbali ardhini.

Nadharia nyengine inayoelezea chanzo cha samaki hao kuangua ardhini kutoka mbinguni ni ile isemayo kuwa, “Mvua ya Samaki” husababishwa na upepo wa “uzumui” wa majini hasa baharini ambazo husababishwa na mbinyo wa hewa katika usawa wa bahari.

Kama ilivyo kawaida ya upepo wa uzumui ambao huvuma kwa kuzunguuka kwa kasi kubwa, upepo huo huchukua kima kingi cha maji na kuyapandisha hewani yalizunguuka na upepo huo unaopaa juu angani.

Kutokana na nguvu za upepo huo, mbali ya kuchukua maji mengi na kuyapandisha juu angani, lakini pia husomba aina mbalimbali za vitu vilivyo karibu na unapovuma upepo huo.

Katika mazingira hayo, ndipo samaki wengi walio majini huchukuliwa na upepo huo mkali wa uzumui unaozunguka na kuwapandisha hewani samaki hao wengi.

Kwa vile upepo huo hutoka baharini au ziwani na kuelekea nchi kavu, kadiri unavyo karibia ardhini na nchi kavu huku ukiandamana na mvua kubwa yenye dhoruba hupungua kasi na ndipo samaki hao ambao walipandisha hewani na upepo huo huanguka ardhini.

Hata hivyo, kinyume na nadharia mbili hizo, baadhi ya wanasayansi wanadhani kuwa katika kijiji hicho cha Yoro nchini Honduras kuna bwawa, panga, ziwa au eneo kubwa la maji lilioko chini ya ardhi ambako samaki hao wanaishi.

Samaki hao hulazimika kutoka sehemu hiyo pale mafuriko yanapotokea kwa vile sehemu hiyo wanayoishi hujaa maji na kuwaburura samaki hao hadi juu ya ardhi. Hata hivyo pia maelezo hayo yanazua masuala kadhaa yasiyo na majibu kwa vile si rahisi kuwepo sehemu chini ya ardhi ya kijiji hicho yenye kuishi samaki wengi ambayo haijulikani wapi ilipo kwa zaidi ya miaka 200 sasa tokea samaki hao walipoanza kuanguka ardhini kwa wingi.

Hata hivyo licha ya nadharia zote hizo tofauti za wanasayansi kuhusiana na samaki hao, Watu wa Yoro tokea mwaka 1998  wamekuwa wakifanya sherehe kubwa wanapoanguka samaki hao ambapo sanamu la Padri Jose Manuel hutembezwa katika mji huo ikiwa ni kumbukumbu ya kumuenzi Padri huyo kwa kile kinachoaminika kuwa yeye ndiye aliyemuomba Mungu na kuteremsha samaki hao katika miaka 1850.