NA KHAMISUU ABDALLAH

MWANAMAMA aliyedaiwa kumtafuna mwenziwe katika bega, amefikishwa katika mahakama ya wilaya Mwanakwerekwe.

Mshitakiwa huyo alitambulika kwa jina la Fatma Salum Ali (31) mkaazi wa Magomeni wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Akiwa katika kizimba cha Hakimu Suleiman Said Suleiman na kusomewa shitaka lake na Mwendesha Mashitaka, Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya DPP, Nassra Khamis, kuwa mshitakiwa huyo alipatikana na kosa la shambulio la hatari kinyume na kifungu cha 208 cha sheria ya adhabu namba 6 ya mwaka 2018 sheria za Zanzibar.

Mshitakiwa huyo alidaiwa kuwa bila ya halali alimshambulia kwa hatari Zainab Bakar Abdalla, kwa kumtafuna katika bega lake la kulia kitendo kilichopelekea kumsababishia madhara mwilini mwake.

Tukio hilo alidaiwa kulitenda Ogasti 5 mwaka jana majira ya saa 4:00 asubuhi huko Magomeni Kwamtumwa Jeni wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Mshitakiwa huyo aliposomewa shitaka hilo alilikataa na kuiomba mahakama impatie dhamana, huku upande wa mashitaka ukidai kuwa upelelezi wake tayari umeshakamilika na kuomba kupangiwa tarehe nyengine kwa ajili ya kuwasilisha mashahidi.

Hakimu Suleiman alikubaliana na ombi la upande wa mashitaka na kuiahirisha kesi hiyo hadi Januari 14 mwaka huu na kuamuru upande wa mashitaka kuwasilisha mashahidi siku hiyo.

Mahakama ilimtaka mshitakiwa huyo kujidhamini mwenyewe kwa shilingi 300,000 za maandishi na kuwasilisha wadhamini wawili, ambao kila mmoja atamdhamini kwa kima hicho hicho cha fedha pamoja na kuwasilisha barua na kitambulisho kinachotambulika.

Mshitakiwa huyo alikamilisha masharti hayo na yupo nje hadi tarehe nyengine aliyopangiwa mahakamani hapo kwa ajili ya kusikilizwa ushahidi.