NA ASIA MWALIM

MKURUGENZI Idara ya Watu Wenye Ulemavu Zanzibar, Abeda Rashid Abdallah, amewataka wadau na watu mbalimbali wenye uwezo kujitokeza na kuwasaidia watu wenye ulemavu, ili waweze kujiinua kiuchumi na kupata maendeleo.

Aliyasema hayo wakati wa ziara ya kukabidhi msaada wa vitu mbalimbali ikiwemo nguo kwa watu wenye ulemavu, vyenye thamani ya shilingi millioni 20 huko Baraza la mji, Wilaya ya kati Unguja.

Mkurugenzi Abeda alisema, endapo wafadhili wataendelea kujitokeza kuwawezesha watu wenye ulemavu kutasaidia kutatua changamoto zinazowakabili katika mahitaji yao ya msingi ikiwemo kupata elimu, chakula na mavazi.

Alifahamisha kuwa watu wenye ulemavu hupata matumaini pale wanapopata misaada au kupewa zawadi, ambazo mara nyingi huwafariji na kuona ni jinsi gani jamii inavyowajali.

Alieleza kuwa licha ya viongozi wa Serekali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuendelea kutoa mahitaji ya watu hao, pia ipo haja kwa wadau kutoa mashirikiano yao ukizingatia mahitaji ya watu hao ni mengi.

Aidha, aliwapongeza watendaji wa Baraza hilo kwa mashirikano yao sambamba na kuwataka kutoa taarifa za watu wenye ulemavu kwa maafisa wa Idara hiyo, ili waweze kuzifikisha sehemu husika.

“Kila Wilaya tuna maofisa wetu kwa ajili ya watu wenye ulemavu tungeomba kupeleka taarifa zenu, ili kujua jinsi gani tunaweza kuzipatia ufumbuzi mapema” alisema Abeda.

Mapema Mkuu wa Wilaya Kaskazini ‘B’ Unguja Aboud Hassan Mwinyi, alisema kama ilivyo lengo la kuletwa kwa msaada huo ni kuwafikia watu wenye ulemavu, hivyo atahakikisha unawafika wahusika kwa wakati.

Aidha alieleza kuwa changamoto zinazowakumba watu hao ni nyingi, ikilinganishwa na hali duni ya maisha hivyo kupatiwa misaada husaidia katika kuimarisha maisha yao.

Subira Khamis Yussuf mkaazi wa Dunga, mama mwenye watoto wawili wenye ulemavu, alipokea msaada na kuwashukuru wafadhili waliotoa msaada huo, sambamba na kuwataka wazazi wenye watoto wenye ulemavu kuacha kuwaficha na badala yake kuwapa haki za msingi kama ilivyo kwa watoto wengine.

Nae Msaidizi Mkurugenzi Idara ya masuala ya mtambuka Baraza la mji kati Makame Hassan Mussa, aliishukuru idara hiyo kwa kuwapatia misaada hio na kuiomba Serekali na wadau wengine kuwasaidia zaidi watu hao waweze kufikia malengo.

“Kwa niaba ya Baraza la mji kati tunaomba misaada hii iwe endelevu kutolewa ili iwanufainishe watu wote wenye ulemavu” alisema.

Msaada huo ulitolewa katika Wilaya ya Kati, Kusini na Kaskazini Unguja, ulijumuisha nguo mchanganyiko za kike na kiume, mashuka na pempas, ikiwa ni udhamini kutoka katika jumuia ya Noah Development services Foundation kutoka nchini Korea.