LAILA KEIS NA ASIA MWALIM

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Jamal Kassim Ali, amesema serikali ina matarajio makubwa ya makusanyo ya kodi na kuimarika kwa huduma za mawasiliano kupitia kampuni za mitandao ya simu zilizopo nchini.

Jamal alieleza hayo wakati alipokutana na viongozi wa kampuni za simu za mkononi Zantel na Tigo, waliofika ofisi za wizara hiyo, Vuga mjini Unguja kuutambulisha muungano wa kampuni hizo.

Waziri Jamal alizipongeza kampuni hizo kwa uamuzi waliochukua na kueleza kuwa hatua hiyo itachochea kasi ya maendeleo ya huduma za mawasiliano kwa jamii sambamba, kuongeza mapato na kukuza uchumi wa nchi.

Aidha alisema, serikali ambayo mbia wa kampuni hizo, ina matarajio makubwa ya kukua kwa mapinduzi ya teknolojia kutokana na muungano wa kampuni hizo jambo litakalokuza pato la nchi kupitia mawasiliano.

Alisema teknolojia ya mawasiliano imerahisisha maisha katika jamii, ambapo ukuaji mkubwa wa kiuchumi unatokana na teknolojia ya habari na mawasiliano.

“Mfumo wa malipo kupitia mitandao ya simu, umechangia kwa kiasi kikubwa katika ufanyaji wa biashara na kufikisha huduma katika maeneo ambayo huduma za kifedha zilikua si rahisi kupatikana,” alisema.

Naye Mkurugenzi wa Bodi ya Wadhamini wa kampuni hizo iliyoundwa baada ya muungano huo, Balozi Ameir Mpunwae, alisema,muungano huo ni moja ya mikakati ya kuhakikisha sekta ya mawasiliano nchini inasaidia kwa kiasi kikubwa kasi ya maendeleo ya shughuli mbali mbali za kiuchumi na kijamii.

Balozi Mpunwae alieleza kuwa ulimwengu hivi sasa umeingia katika mapinduzi ya nne ya kidigitali, ambayo sekta ya mawasiliano ina nafasi kubwa ya kukuza ufanisi kama vile upatikanaji wa ajira sambamba na kulipa kodi ipasavyo.

“Kampuni zetu zimechangia kwa kiasi kikubwa kurahisisha miamala ya kifedha na mchango wa ajira sambamba na kuutambua wajibu wetu kwenye kutoa kodi ili kuhakikisha serikali inaendesha shughuli zake za kuleta maendeleo kwa jamii,” alieleza balozi Mpumwae.

Akizungumzia muungano huo afisa mtendaji mkuu wa  Zantel, Brian Karokola, alisema mtandao wao upo tayari kufanya kazi na serikali ili kuhakikisha wanainua uchumi wa nchi.

Kauli hiyo iliungwa mkono na Afisa Mtendaji Mkuu wa Tigo, Simon Karikari, aliyeongeza kwa kuahidi kuwa watatoa ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha kampuni zao zinafikia malengo ya serikali ya kukuza mapato ya nchi na malengo ya kampuni hiyo.