HIVI karibuni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi alikutana na wadau kusikiliza ukubwa wa changamoto ya vitendo vya udhalilishaji.

Mkutano wa Dk. Mwinyi na wadau wa kupambana na vitendo vya udhalilishaji umekuja wiki chache baada ya kumalizika kwa siku 16 za kupinga vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia.

Zanzibar ina changamoto kubwa ya vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia hasa kwa wanawake na watoto kiasi kwamba kila familia inakodoa macho mawili dhidi ya ulinzi wa watoto kwa mafisadi wanaowania kuwaharibu.

Ukweli ni kwamba udhalilishaji wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto limekuwa jinamizi linaloitesa jamii yetu katika miaka ya hivi karibuni huku jamii ikijiuliza masuali mengi kulikoni?

Kwa hakika vitendo hivi jinsi vinavyoendelea kushamiri kwa kasi ya ajabu kila uchao, taarifa za vyombo vya habari hazitoi picha nzuri kwani zinaonesha wananchi wakilalamikia na kuchoshwa navyo.

Licha ya wanaharakati kuandaa mijadala, makongamano yanayoonesha pia takwimu za matukio haya na hatua zinazochukuliwa, bado wahusika wamefumba macho na kutia pamba masikio kama vile wamekumbwa na pepo mbaya.

Kelele, vilio na makaripio mengi mfululizo yanayotolewa kuwasema waovu wanaojihusisha na vitendo hivyo, bado wao wamekuwa kama wanatuambia kwa kejeli, “yaguju, mtasema mchana usiku mtalala”.

Ni ukweli usio shaka kwamba bado sauti zetu za kila siku hazijaingia ipasavyo masikioni mwa watendaji wa matendo hayo na tunajiuliza dawa gani itakayowafaa wahalifu hawa?

Pamoja na wanajamii wengi kuvinyoooshea kidole vyombo vya sheria kwa kudai ama vinatoa adhabu ndogo kwa watu wanaopatikana na hatia au kuzitupilia mbali licha ya kuwepo ithibati za kutosha, lakini nao pia wanapaswa kubeba lawama kwani mara nyingi hutawaliwa na muhali na kumaliza mambo kienyeji au kwa kupokea fedha.

Aidha, mara nyengine jamii hiyo hiyo hulalamika kwamba inavunjwa moyo na vyombo vilivyowekwa kutoa haki kutokana na nenda rudi na panda shuka ngazi zisizokwisha hata pale ushahidi ukiwemo wa watoto wanaoathiriwa unapokuwa wazi na usio na shaka.

Tusingependa kuvilaumu moja kwa moja vyombo vya sheria tunaelewa kwamba kila kesi ina namna na mahitaji yake ya msingi katika kuishughulikia, lakini inavishauri vyombo hivyo vijiweke sehemu ya watendewa wa ukatili huo ili viyahisi machungu yake.

Kwa hali ilivyofika sasa, ni lazima serikali na vyombo vya dola vikubaliane kuchukua maamuzi magumu ikiwemo kuundwa kwa mahakama maalum ambayo itakuwa kazi yake kuendesha kesi hizo kwa haraka zaidi.

Aidha haitoshi kushiriki maandamano, kusikiliza hutuba na kupiga kofi, bali kila mmoja aamue kushiriki kikamilifu katika vita hivi vigumu na awe na mipango namna ya tutakavyoshinda.

Lazima ufike wakati tuthamini juhudi zinazochukuliwa na serikali hasa hii ya awamu ya nane ambapo Dk. Hussein Ali Mwinyi, aliyesema wazi kwamba anakerwa na vitendo hivyo na kutaka ushirikiano wa kutosha kuvikomesha.

Iwapo sote tutaunganisha nguvu na kupambana kwa dhamira ya kweli na vitendo badala ya maneno matupu, Zanzibar bila udhalilishaji wanawake na watoto inawezekana.