HUKU Ligi Kuu ya Zanzibar ikiendelea kuchanja mbuga na kuingia mzunguko wa pili, klabu zimeendelea kupaza kilio chao cha kukosekana kwa udhamini kwenye ligi hiyo kubwa nchini.


Huko nyuma, tuliwahi kuchapisha habari juu ya Chama cha Soka Zanzibar (ZFF), namna kinavyoendelea kutafuta wadhamini ili kukuza ushindani na kuzipunguzia mzigo wa gharama klabu zinazoshiriki ligi hiyo.
Zanzibar Leo kama wadau wa michezo tunaungana na klabu hizo na ZFF kwa ujumla katika kuona udhamini unapatikana kwa ajili ya kuhakisha ligi inakuwa ya ushindani ili kutoa wawakilishi bora wa kimataifa.


Ni ukweli usiopingika kuwa ZFF inapita kwenye kipindi kigumu cha kusimamia ligi hiyo kutokana na kutokuwepo kwa mdhamini rasmi na hivyo kuzifanya klabu kubeba mzigo mzito wa ushiriki wao.


Kama inavyoeleweka ligi ya mwaka huu yenye timu 12, imeendelea kuchezwa kwa mtindo wa nyumbani na ugenini na hivyo kuzifanya timu kusafiri kati ya Unguja na Pemba katika kukamilisha ratiba ya ligi hiyo.
Sote ni mashahidi kuwa klabu zetu hazipo vizuri kiuchumi na zinaendeshwa kupitia michango ya mashabiki au viongozi wanaoziongoza hali ambayo kidogo inaweza kuweka rehani ushiriki wao pale michango itakapokosekana.


Kwa maana hiyo, iwapo itatokezea timu ikashindwa kuendelea na ligi jambo ambalo hatuliombei kutokea, kunaweza kuvuruga mwenendo mzima wa ligi hasa ikizingatiwa kwamba timu inaposhindwa kutokea kwenye michezo mitatu mfululizo inakuwa tayari imejiondoa kulingana na kanuni za mashindano.


Hivyo, tunaamini kupatikana kwa mdhamini ambaye kwa kiasi fulani atasaidia uendeshaji wa ligi hiyo na klabu kuweza kushiriki bila ya gharama kubwa, ni miongoni mwa mambo yanahitaji kufanyiwa kazi kwa kadri ya iwezekanavyo.


Ni jambo zuri kuliona soka likichezwa kwenye utaratibu unaokubalika viwanjani huku wachezaji wakitimiza majukumu yao jambo ambalo litaifanya ligi kuwa ya ushindani zaidi badala ya kuonekana ligi iliyokosa dira.
Kama ambavyo wanafalsafa wa kiswahili wanavyosema kuwa mchezo ni gharama, basi sote tulione hilo kwa kuiunga mkono ZFF iweze kufanikiwa kupata mdhamini kwa ajili ya maendeleo ya soka yetu.


Kwa kipindi kirefu sasa Ligi Kuu ya Zanzibar imekuwa ikichezwa bila ya udhamini, labda kutokana na mfumo uliokuwepo kabla ambao pia ulichangiwa na idadi kubwa ya timu shiriki.


Lakini tunaamini kwa mfumo wa sasa, udhamini unawezekana hasa ikizingatiwa huko mbele tunakoelekea idadi ya timu itaendelea kushuka kutokana na mfumo unaokusudia kuwekwa na ZFF.


Sasa tufikie mahali na kuliona hili ni letu sote kwa njia moja au nyengine ili siku ya mwisho ligi yetu iwe na udhamini utakaongeza chachu ya mafanikio kwa ajili ya vijana wetu wa baadaye.
Zanzibar yenye mafanikio ya soka inawezekana.