UTAFITI mpya uliotolewa na Chuo Kikuu cha Cambridge cha nchini Uingereza unaonesha kuwa viumbe walioishi katika kipindi cha kale duniani walibadilika na kuwa warefu na wakubwa zaidi.

Watafiti hao walieleza sababu ya mabadiliko hayo si kusaidia kutafuta chakula, bali ni kueneza vizazi vijavyo katika eneo kubwa zaidi na kuzaliana kwa ufanisi mkubwa zaidi.

Ripoti iliyotolewa kwenye jarida la Nature Ecology & Evolution inasema kabla ya kipindi cha Sinian (miaka milioni 635 hadi miaka milioni 541 iliyopita), viumbe walikuwa wadogo sana.

Lakini baada ya kuingia kipindi cha Sinian, viumbe wakubwa walianza kutokea, hata urefu wao ulifikia mita mbili na ingawa walifanana na mimea aina ya fern, lakini huenda ni wanyama wa kale zaidi duniani.

Watafiti wanaona kuwa viumbe wanaozaliana baharini walijaribu kueneza vizazi vijavyo mbali zaidi na kuanzisha makazi yao huko na wale wakubwa walikuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kutimiza lengo hili.

Kabla ya hapo, wanasayansi walifikiri viumbe wakubwa walikuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kutafuta chakula.

Mwandishi wa ripoti hiyo alisema wakati huo kulikuwa na vyakula vingi baharini, viumbe hawakukabiliwa na shinikizo kubwa la kutafuta chakula, hivyo ukubwa wao hauhusiani na kutafuta chakula, bali unahusiana na kuzaliana.