HUWA ni jambo la kawaida kuwaona watoto wadogo wakinyonya kidole gumba cha mkono. Ingawa katika jamii zetu zilizo nyingi jambo hili huonekana baya na hukemewa na mara nyingi mtoto anayefanya hivi huadhibiwa kwa bakora na adhabu zingine mfano wa huu.

Makala haya yanalenga kukupatia sababu za kitaalamu za kwa nini jambo hili hutokea na kukupa mbinu mbadala za kusaidia kukomesha tabia hii.

Moja ya sababu za watoto kunyonya kidole gumba ni faraja na utulivu wa mawazo unaopatikana wanapofanya hivi. Inayumkinika kuwa mwanao yawezekana alianza kunyonya kidole akiwa bado angali tumboni mwa mama yake na mpaka anazaliwa alishakuwa mbobezi katika tabia hii.

Mara nyingi mtoto hunyonya kidole gumba awapo na uchovu, hofu, ‘kuboreka’, mgonjwa au kujaribu kuzikabili changamoto mbalimbali kama vile kuanza kwenda shule ya chekechea au awapo katika safari ndefu.

Vilevile mtoto hutumia unyonyaji wa kidole gumba punde anapohisi kutaka usingizi ama ‘kujibembeleza’ wakati anaposhtuka usingizini katikati ya usiku.

Sasa unajua kwa nini mtoto wako ananyonya kidole chake, jjiunge nasi hapa chini katika safari ya kupambana na tabia hii bila ya kuathiri ukuaji mwema wa mtoto.

Usiwe na wasiwasi. Watoto wengi wanaweza kunyonya kidole gumba kwa usalama tu bila kuharibu mpangilio wa meno yao au taya mpaka wakati meno yao ya kudumu yanapoanza kuota wakiwa karibu na umri wa miaka sita. Vilevile, si kweli kwamba wote wanaonyonya vidole huleta madhara.

Watoto wanaonyonya kidole bila kukikandamiza hupunguza madhara kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na wenzao wanakandamiza kidole wakati wakikinyonya. Mwangalie mwanao, je ananyonya kidole kwa nguvu ama hatumii nguvu.

Iwapo anatumia nguvu (kukandamiza kidole), unashauriwa kuanza kupambana na tabia hii mapema akiwa na umri wa kuanzia miaka minne.

Usimwadhibu mtoto. Kumgombeza na hata kumwadhibu mtoto wako haitasaidia, kwani mara nyingi huwa hajui wala kukumbuka kuwa tayari ananyonya kidole. Hili huwa ni tendo linalokuja pasi hiari wala kuwaza kwake.

Mbali na hilo, uzoefu unaonyesha kuwa ukimshinikiza aache inaweza kuchangia yeye kutaka kufanya hivyo hata zaidi na zaidi. Vilevile mbinu kama kuweka plasta juu ya kidole gumba chake, kuweka pilipili, nk. ni uonevu usiokuwa na msingi hasa kwa sababu unajua yeye hufanya kitendo hiki kwa ajili ya faraja na usalama. Jaribu kuwa na subira.

Kawaida watoto huachana na tabia hii wenyewe wakati wameweza kujitambua na kupata njia mbadala ya kujieleza, kujiletea utulivu na faraja. Kwa mfano, wakati mwanao mdogo awapo na njaa hunyonya kidole, mtoto wako mkubwa (mwenye umri wa miaka mitatu au minne) yeye anaweza kukwambia kuwa ana njaa ili umpe chakula.

Mpe Mbadala. Pale unapojua kwamba mtoto wako atapata sababu za kunyonya kidole, jaribu kumpa shughuli mbadala. Wakati wa kuangalia televisheni, kwa mfano – unaweza kumpa mdoli/mwanasesele kubinyabinya hii itapunguza au kuhamisha mawazo yake.

Unapojua kuwa akichoka hunyonya kidole basi ongeza vipindi vya kulala katika ratiba yake ya siku. Au kama yeye hufanya tabia hii awapo na hasira, msaidie kujua namna ya kujieleza awapo na hasira (kuweka hisia zake katika maneno). Jambo la muhimu ni kujua kwa nini na ni muda gani mwanao hufanya tabia hii ili utumie njia sahihi kumpa mbadala.

Mwisho kabisa iwapo kidole gumba cha mtoto wako kitakuwa chekundu kutokana na kunyonywa, jaribu kutumia vilainishi maalumu (vipo madukani) wakati akiwa emelala. Kamwe usimpake vilainishi akiwa macho kwani dawa yote hii itaishia mdomoni mwake kwa kunyonywa.

Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org